Kijana Shadrack Yusuph Chaula (24) mkazi wa kijiji cha Ntokela kata ya Ndanto Tukuyu wilayani Rungwe, ameachiwa huru kutoka mikononi mwa jeshi la magereza baada ya kufanikiwa kulipa faini ya shilingi million tano kutokana na hatia aliyokutwa nayo ya udanganyifu juma lililopita.
Kijana Shadrack Chaula amelipa fedha hizo baada ya kuchangwa na wanaharakati na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Chaula alihukumiwa na mahakama ya wilaya ya Rungwe kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya shilingi million tano baada ya kukiri kosa la kuandaa na kusambaza taarifa za uongo.
Baada ya hukumu hiyo juma lililopita, kijana huyo alienda gerezani kuanza kutumikia kifungo cha miaka miwili jela ndipo baadaye wanaharakati wakaanzisha mchango ili kupata fedha za kumtoa gerezani na kufanikiwa kupata zaidi ya shilingi million sita.
Jopo la mawakili na watu mbalimbali wamefika katika viunga vya magereza ya Ruanda jijini Mbeya ambapo baada ya kushughulikia mambo kadhaa kijana Shadrack Chaula ameachiwa na kwenda kuendelea na maisha yake ya kawaida.
Baada ya kutoka gerezani Shadrack Chaula amewashukuru wananchi wote kwa kuungana naye na kumsaidia kuhakikisha anatoka gerezani.
Wakili wa kujitegemea Michael Mwangasa, amesema wameshirikiana kuona kijana huyo anaachiwa huru kwa kulipa faini tajwa na mahakama.
CHANZO - MATUKIO DAIMA MEDIA
Naye Twaha Mwaipaya kwa niaba ya walioanzisha ukusanyaji fedha hizo, ameushukuru umma wa wa-Tanzania kwa kuungana kuhakikisha kijana huyo anaepuka adhabu ya jela.