ASKOFU SANGU AMSHUKURU MUNGU KWA KUTIMIZA MIAKA 30 YA UPADRE

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, ameongoza Misa ya kumshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 30 tangu alipopewa Daraja la Upadre, katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga.
Askofu Sangu ametumia nafasi hiyo kuomba neema na Baraka za Mwenyezi Mungu ili amjalie nguvu ya kuendelea kumtumikia kwa uaminifu, akifuata mfano wa Kristo ambaye ni mchungaji mwema.
Amewashukuru wote waliochangia kufikia Daraja la Upadre, wakiwemo wazazi wake ambao wametangulia mbele za haki, viongozi wa Kanisa na watu wote wenye mapenzi mema.
Askofu Sangu amelielezea Daraja la Upadre kuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu mwenyewe, ambalo limemwezesha kuwa sehemu ya warithi wa kazi ya mitume ya kumtangaza Kristo na kumpeleka kwa watu.
Wakati huohuo, Askofu Sangu amewataka Wakristo wote kuendelea kuombea Amani ya dunia pamoja na kuishi maisha ya kumshuhudia Kristo, wakikomesha ubinafsi na kuonesha upendo kwa wengine, pamoja na kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya watu wenye uhitaji.
Askofu Sangu alipewa Daraja la Upadre mnamo Julai 3 mwaka 1994, katika Jimbo Katoliki Sumbawanga, ambako alifanya utume katika idara na Parokia mbalimbali za Jimbo akiwa mmoja wa Mapadre wa Jimbo hilo, kabla ya kutumwa Vatican alikofanya kazi kama Afisa Mwandamizi kwenye Idara ya Uinjilishaji wa watu.
Akiwa Vatican, Baba Mtakatifu Francisco alimteua kuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga, mnamo Februari 2 mwaka 2015.

Watu mbalimbali wakiwemo Mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini ambaye pia ni Naibu waziri ofisi ya Waziri Mkuu, kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu Paschal Patrobas Katambi pamoja na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga Janeth Magomi wampongeza na kumtakia matashi mema Askofu Sangu kwa kutimiza kwake miaka 30 ya Upadre. 

Previous Post Next Post