Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amemteua Padre Richard Makoye kuwa Katibu wa Askofu na mthibitishaji wa nyaraka muhimu za kuria ya Kanisa (Chancellor)
Padre Makoye ambaye amemaliza masomo yake ya Shahada ya uzamili ya Theolojia ya Maadili huko Roma nchini Italia, ametangazwa kushika majukumu hayo leo mara baada ya Misa ya utolewaji wa Daraja Takatifu la Upadre kwa waliokuwa Mashamasi 11 wa Jimbo, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Bikra Maria Mediatrix Buhangija mjini Shinyanga.
Askofu Sangu pia amemteua Padre Richard Makoye kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Ngokolo mjini Shinyanga ambapo Padre Paschal Kassase ameteuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Ndala mjini Shinyanga, ambaye atasaidiwa na Padre Sylvanus Kidaha pamoja na Padre mpya Musa Majura.
Aidha, Askofu Sangu amemtaja Padre Paul Mahona kuwa ataendelea kuwa Paroko wa Parokia ya Ndembezi iliyopo mjini Shinyanga.
Wakati huohuo, Askofu Sangu amemtuma Padre Deusdedith Tungu aliyehitimu masomo ya Kiarabu na Kislam huko Roma kwenda kuwa Mkufunzi katika Seminari kuu ya Peramiho iliyopo Jimbo kuu la Songea, baada ya kuombwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC.