Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kesho Jumatano tarehe 03.07.2024, ataongoza Misa ya kumshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 30 ya Upadre.
Misa hiyo itanyika katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga, kuanzia saa 3:00 asubuhi na itahudhuriwa na Mapadre, Mashemasi, Mafrateri, watawa na waamini kutoka sehemu mbalimbali za Jimbo.
Misa hiyo itafuatiwa na tafrija fupi ya kumpongeza Askofu sangu, ambayo itafanyika saa moja jioni kwenye makazi ya Askofu Ngokolo mjini Shinyanga.
Askofu Sangu alipewa Daraja la Upadre mnamo Julai 3 mwaka 1994, katika Jimbo Katoliki Sumbawanga, ambako alifanya utume katika idara na Parokia mbalimbali za Jimbo akiwa mmoja wa Mapadre wa Jimbo hilo, kabla ya kutumwa Vatican alikofanya kazi kama Afisa Mwandamizi kwenye Idara ya Uinjilishaji wa watu.
Akiwa Vatican, Baba Mtakatifu Francisco alimteua kuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga, mnamo Februari 2 mwaka 2015.
Mapadre, Mashemasi, Mafrateri, watawa na waamini wanamtakia matashi mema katika utume wake wa kulichunga jimbo Katoliki la Shinyanga.