Ticker

6/recent/ticker-posts

ASKOFU SANGU KUZINDUA PAROKIA MPYA YA LAGANGABILILI

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, kesho Ijumaa tarehe 05.07.2024, atazindua Parokia  mpya ya Lagangabilili iliyopo makao makuu ya Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, ikiwa ni mwndelezo wa mpango wake wa kusogeza huduma za kiroho kwa waamini.

Uzinduzi wa Parokia hiyo ambayo imetokana na kumegwa kwa sehemu ya Parokia kongwe ya Kilulu, utafanyika kwa Misa takatifu ambayo itafanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Paulo wa Msalaba kuanzia saa 4:00 asubuhi, itakayohudhuriwa na Mapadre, watawa, Mashemasi, Mafrateli na waamini kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Jimbo la Shinyanga, wakiwemo viongozi mbalimbali wa Serikali.

Uzinduzi huo utakwenda pamoja na utolewaji wa Sakramenti ya kipaimara kwa waimarishwa 275 pamoja na kubariki ndoa zipatazo nne.

Askofu Sangu atawasili katika Parokia teule ya Lagangabillli leo Alhamisi, ambapo pamoja na mambo mengine, ataweka jiwe la msingi na kubariki shule mpya ya mchepuo wa kiingereza ya Parokia hiyo teule, iliyopewa Jina la Bishop Sangu Nusery & Primary school.

Kuanzishwa kwa Parokia mpya ya Lagangabilili, kunalifanya Jimbo Katoliki Shinyanga kuwa na Jumla ya Parokia 40 kutoka 39 za sasa, ambapo Askofu sangu atakuwa ameongeza Jumla ya Parokia 14 kwa kipindi chake cha miaka 9 tangu alipowekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Shinyanga, kutoka Parokia 26 alizozikuta.

Parokia mpya ambazo zimeanzishwa na Askofu Sangu ni pamoja na Ngulyati, Bukundi, Old Shinyanga, Nindo, Ndala, Kitangili, Mhunze, Mtakatifu Luka-Bariadi, Lubaga, Maganzo, Luguru, Shishiyu, Ndembezi na Lagangabili ambayo itazinduliwa rasmi hapo kesho.

Post a Comment

0 Comments