SERIKALI imesema imekamilisha kanzidata ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya na imeanza uchunguzi wa watu hao, huku Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ikisema kila siku inapokea waraibu 900 wanaotumia dawa za usaidizi wa kuacha matumizi ya dawa za kulevya ‘methadone’.
Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wa waandishi wa habari na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, pamoja na Mkurugenzi wa MNH, Prof. Mohamed Janabi.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulikuwa na lengo la kutoa taarifa kuhusu kukamatwa kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Prof. Janabi alisema: “Ukubwa wa hili tatizo (matumizi ya dawa za kulevya), ni kubwa sana. Kwenye kanzi data yetu (MNH) hadi Juni, mwaka huu watu 3,840 wanapata tiba ya dawa ya methadone pale Muhimbili.”
Alisema kila siku watu 900 wanakuja kunywa tiba ya methadone MNH, kwamba ndiyo kituo chenye watu wengi walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya kuliko sehemu yoyote hapa nchini.
Alisema dawa za kulevya zina athari nyingi mojawapo ni kuharibu mfumo wa umeme wa moyo na ndiyo sababu vijana wengi wanapata matatizo na kusababisha vifo vya ghafla.
Pia, zinaharibu figo, akitoa takwimu kwamba MNH inasafisha wagonjwa 150 kwa siku wenye matatizo ya ugonjwa huo, ambao wanahudumiwa kwa vipindi vitatu.
Kadhalika, alisema wanaotumia dawa za kulevya wanapata ugonjwa wa saratani kwa sababu wanachangia sindano na kupata homa ya ini, baadhi yao wanaugua saratani ya ini.
WAFANYABIASHARA KUKAMATWA
Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema mamlaka hiyo imemkamata mkazi wa Jiji la Dar es Salaam, Shaban Adam (54) kwa tuhuma za kutengeneza dawa za kulevya.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa nyumbani kwake Juni 11, mwaka huu, akitengeneza dawa za kulevya aina ya heroin kwa kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya, akichanganya na kemikali bashirifu.
Pia alisema DCEA inamshikilia, Mbaba Issa ambaye alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Melchior Ndadaye Bujumbura, Burundi akielekea Dubai akiwa na kilo 3.8 za dawa za kulevya aina ya skanka.
Vilevile, alisema DCEA ilifanya operesheni katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Mtwara na Mbeya na kukamata magunia 285 ya bangi, kilo 350 za dawa za kulevya, milimita 115 za dawa tiba zenye asili ya kulevya pamoja na lita 19,523 za kemikali bashirifu.
Alisema katika operesheni hiyo watuhumiwa 48 wamekamatwa na watafikishwa katika vyombo vya sheria.
KANZI DATA
DCEA imekamilisha kanzi data ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya pamoja na kuanza uchunguzi kuhusu watu hao.
“Wengi wamebainika wapo ndani ya nchi na wengine nje ya nchi. Baadhi yao wana biashara nyingine halali, lakini wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kufanya utakatishaji,” alisema.