Na Respice Swetu, Kasulu
Ikiwa ni
siku moja baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Philip
Isidor Mpango kutoa agizo kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya
Kasulu kufanya mkutano na wakazi wa kijiji cha Nyakitonto kilichopo kwenye
halmashauri hiyo, agizo hilo limetekelezwa.
Kufuatia
agizo hilo, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Dr. Mashimba akifuatana
na wataalamu kutoka katika ofisi yake, amezungumza na wakazi wa kijiji cha
Nyakitonto katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo.
Katika mkutano
huo wakazi wa kata ya Nyakitonto wakiongozwa na diwani wa kata hiyo Daniel
Nzababa, pamoja na kupata fursa ya kufahamiana na mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri ya wilaya ya Kasulu, waliutumia mkutano huo pia kuwasilisha hoja
mbalimbali za kujiletea maendeleo.
Miongoni mwa
hoja zilizowasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na zilizohusu ardhi, huduma
za afya, huduma za maji, huduma elimu, kilimo, hifadhi ya mazingira,
miundombinu na ushirikishwaji.
Akijibu hoja
hizo Dr. Mashimba ambaye amehamia katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu hivi karibuni
kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino iliyopo mkoani Dodoma amesema,
lengo lake ni kuiona Nyakitonto na halmashauri nzima ya wilaya ya Kasulu inapata
maendeleo.
Ili
kuyafikia maendeleo hayo Dr. Mashimba amesema, hatua mbalimbali zinapaswa
kuchukuliwa.
Dr. Mashimba
amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kutenga maeneo yatakayotumika kwa ajili
ya kujenga viwanda na taasisi mbalimbali kama mabenki, TRA, maduka, sehemu ya
kuegesha malori na kituo cha biashara.
Dr. Mashimba
amewatahadharisha wakazi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu kuwa katika kuyafikia
maendeo hayo kuna gharama.
Amezitaja
baadhi ya gharama hizo kuwa ni pamoja na kutoa ardhi kwa ajili ya upitishaji wa
miundombinu ya barabara, maji na kuchangia zoezi la urasimishaji na mpango bora
wa matumizi ardhi.
Pamoja na
mkutano huo kufanyika kutokana na maagizo ya Makamu wa Rais, tangu kufika kwake
Dr. Mashimba amekwisha fanya ziara
katika vijiji na kata mbalimbali za halmashauri ya wilaya ya Kasulu kwa lengo la kagua miradi ya maendeleo na
kuzungumza na wananchi.