Mdau mkubwa wa muziki wa dansi nchini Bernard James amewaomba wadau na mashabiki wa muziki wa dansi mkoani Dodoma kuziunga mkono bendi za mkoani humo siku ya tamasha la Usiku wa Wafia Dansi.
Bernard James ambaye pia ni mwanahabari nguli na mkurugenzi wa kampuni ya burudani Cheza Kidansi Entertainment amesema mashabiki wasipofanya hivyo watazivunja moyo bendi za Dodoma na pengine kuzishusha morali.
"Mwaka huu tumewapendelea sana mashabiki wa Dodoma kwa kuzipa nafasi bendi za mkoa huo pekee ili kuona je zina mashabiki wanaozipenda au mpaka wabebwe na bendi kutoka mikoa mingine?"
"Unapoandaa matamasha Dodoma kama tulivyofanya tamasha lililopita, mashabiki hupenda ziwepo bendi kutoka mikoani mfano Dar es Salaam au Arusha au Morogoro, lakini mwaka huu tumeamua kuwapa nafasi ya pekee wanamuziki na bendi za Dodoma pekee ili ziuthibitishie umma kama zinaweza kukusanya vijiji bila wageni"
Bernard ambaye ni mwandaaji pekee wa tuzo pekee za muziki wa dansi nchini pia mdau aliyeleta mapinduzi makubwa kwenye dansi kwa ubunifu mkubwa amesema litakuwa jambo la aibu na kuchekesha kama bendi za Dodoma zitashindwa kuvuna kijiji siku hiyo na kuwavutia mashabiki ambao zinaamini zinao.
"Tamasha hili litakuwa kipimo tosha kwa bendi za Dodoma kuwa je zinatosha? Au mpaka zichomekewe wasanii kutoka nje? Pia kitakuwa kipimo kuwa mashabiki wao wanaowaamini watajaa kuwapa sapoti siku yenyewe?"
Bernard amewaomba wadhamini wengi zaidi kujitokeza kudhamini tamasha hilo ili kuongeza chachu kwa wanamuziki kufanya vizuri zaidi jukwaani
"Mpaka sasa tamasha hili limedhaminiwa na Star TV, Redio Free Afrika, Cheza Kidansi, BJ Fashion na C FM ya Dodoma, tunaomba sana wajitokeze wadhamini wengi zaidi ili kulinogesha tamasha hili na kulifanya liweke rekodi mpya mkoani Dodoma"
Alipoombwa kuwahakikishia mashabiki kama bendi hizo zitatosha kushusha burudani nzito, Bernard amebainisha kuwa bendi zote zipo makini na zina ubora wa kiwango cha juu kutoa burudani tosha bila kubakiza.
Tamasha la Usiku wa Wafia Dansi litafanyika jijini Dodoma katika hoteli ya Royal Village tarehe 2 Agosti huku viingilio vikiwa sh 10,000, sh 30,000 na VVIP 500,000 meza moja viti 10
Tamasha hilo maarufu zaidi nchini limekwishafanyika katika majiji ya Mwanza, Dodoma, Dar es Salaam, Arusha na mjini Morogoro katika misimu mitano mfululizo
Kituo cha Star TV kitarusha tamasha hilo mubashara.