Ticker

6/recent/ticker-posts

HIFADHI SACCOS YANUFAISHA WATUMISHI TANAPA

Meneja wa HIFADHI SACCOS Ibrahim David (wa kwanza kushoto) akiwa na wafanyakazi wenzake katika banda lao kwenye maonesho ya vyama ushirika yanayofanyika katika uwanja vya Fatuma Mwasa Ipuli Mkoani Tabora.


Na Lucas Raphael,Tabora

MFUKO wa Hifadhi Saccos Ltd unaojishughulisha na utoaji mikopo kwa watumishi wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) nchini umewezesha watumishi kupata mikopo nafuu ya zaidi ya sh bil 80 tangu kuanzishwa kwake.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa Taasisi hiyo Ibrahim David alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea banda la Mfuko huo katika Viwanja wa Maonesho ya Ushirika Mkoani Tabora jana.

Alisema kuwa Taasisi hiyo iliyoko Jijini ilianzishwa mwaka 2000 hapa nchini na hadi sasa ina zaidi ya wanachama 1050 na imetoa mikopo nafuu ya maendeleo kwa watumishi walio chini ya TANAPA yenye thamani ya zaidi ya sh bil 80.

Alibainisha malengo makuu ya Taasisi hiyo iliyoko chini ya Wizara ya Mali asili na Utalii kuwa ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi Watumishi wa Hifadhi hizo kwa kuwawezesha kuanzisha miradi ya maendeleo pasipo kutegemea mishahara.

David alifafanua kuwa mikopo inayotolewa huanzia sh mil 5 hadi 20 na hurejeshwa ndani ya miaka 3 na kuongeza kuwa mikopo hiyo imekuwa na manufaa makubwa sana kwani imewawezesha kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Alitaja malengo mengine kuwa ni kuwezesha mwanachama kujiwekea akiba katika mfuko huo au kununua hisa ili atakapostaafu awe na akiba ya kutosha ambayo itamwezesha kuendesha maisha yake vizuri pasipo hofu yoyote.

Alitaja mipango ya baadaye wa Taasisi hiyo kuwa ni kuanzisha miradi ya uuzaji viwanja kwa wanachama wake ili kuwasaidia kujenga nyumba zao kirahisi na kuwekeza katika taasisi nyingine za kifedha kama vile UTT Amis na nyinginezo.

‘Natoa wito kwa watumishi wote wa Uhifadhi (TANAPA) ikiwemo TAWA na TFS kujiunga na mfuko huu ili kunufaika na fursa lukuki zilizopo, ili kujikwamua kiuchumi’, alisema.   

Mwanachama wa Mfuko huo Abushi Shaibu alikiri kuwa tangu ajiunge na Taasisi hiyo amepata manufaa makubwa ikiwemo kujenga nyumba ya kisasa, kuanzisha duka kubwa la nguo, kununua gari zuri na sasa anataka kuanzisha mradi wa kuku.

Joseph Gombeni mkazi wa Arusha naye alisema kuwa Mfuko huo umempa manufaa makubwa sana ikiwemo kusomesha watoto kuanzia shule ya msingi, sekondari hadi chuo kikuu na maisha yake ni mazuri sana.

 

Post a Comment

0 Comments