Kamishna wa Polisi Jamii (CP) Faustine Shilogile ametaja sababu za Jeshi la Polisi kuwa karibu na wananchi baada ya kubaini Jeshi la Polisi pekee haliwezi kuzuia uhalifu kwa kuwa uhalifu ni zao la Jamii, hivyo likaamua kuishirikisha.
Kauli hiyo ameitoa Julai 01, 2024 kata ya Nyantukala, wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza kwenye mkutano wa hadhara alipokutana na Watendaji wa Kata, Maafisa ustawi wa jamii, Wakaguzi kata, watu wenye ualbino, wenyeviti wa vijiji, vikundi vya ulinzi shirikishi, Sungusungu na wananchi.
"Jeshi la Polisi tuliamua kuishirikisha Jamii katika kuzuia uhalifu baada ya kubaini sisi peke yetu hatutaweza kizuia uhalifu, kwa sababu wananchi wapo mbali kidogo na Polisi na ilipofika mwaka 2006 tuliamua kuwa karibu na jamii" amesema Shilogile.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza; Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza wameendelea kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kutoka ofisini na kwenda kutoa elimu katika makundi yote ili usalama uwepo na amani iendelee kutawala.
Kuhusu namna ya kuyalinda makundi maalumu hasa watoto, wazee, akina mama na watu wenye ualbino; kamanda Mutafungwa amesema wameendelea kuwashirikisha Wakaguzi kata na watendaji wa kata katika kudhibiti uhalifu kwa kutoa elimu.
"Kuna operesheni inayoendelea ya kukamata waganga wa tiba asilia wanaofanya vitendo vya ramli chonganishi na operesheni hiyo inaenda sambamba na utoaji wa elimu ya kudhibiti uhalifu" amesema Kamanda Mutafungwa.
Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Faidha Suleiman ameiasa jamii kuwasaidia vijana katika malezi kwani walio wengi bado hawajui kutafsiri makosa kisheria.
"Vijana wengi wanajihusisha kimapenzi na mabinti wadogo wenye umri chini ya miaka 18, kwani ni kosa kisheria" amesema ACP Faidha.
Akiongea kwa niaba, Mwenyekiti wa waganga na wakunga wa Tiba asili Wilayani Sengerema, Shigela Mashimba amesema wapo tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwabaini waganga wa tiba asilia wanaopiga ramli chonganishi huku akiliomba Jeshi la Polisi kuendelea kuwalinda wanaotoa taarifa Ili kuepuka kusababisha migogoro Katika jamii