Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea kufanya uchunguzi katika tukio la Mzee mwenye umri wa Miaka 70 aliyefahamika kwa jina la Christopher Simbila mkazi wa Mtaa Bugweto kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, ambaye amejinyonyonga hadi kufa.
Kwa mujibu wa kaimu
kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi wa polisi Kenedy Mgani,
amesema tukio hilo limegunduliwa na
jirani yake ambapo inasadikiwa mzee huyo amejinyonga jana Jumatatu Julai
1, majira ya asubuhi.
Ameeleza kuwa Mzee huyo
amejinyonga kwa kutumia kamba ya manila ambayo aliifunga kwenye kenchi Sebleni
kwake, hali iliyomsababishia kifo chake papo hapo ,ambapo uchunguzi wa awali
umebaini kuwa huenda kifo cha mzee huyo kimechangiwa na msongo wa mawazo kwa
kuwa alikuwa akisumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.
Misalaba Media, imezungumza
na Mtoto wa Marehemu Bwana Paul Simbila ambaye ameeleza kuwa jana asubuhi
wakati akimpeleka Mtoto wake shuleni, alipita nyumbani kwa Baba yake ili
kumtakia hali lakini alipoingia ndani alimkuta akiwa amejinyonga.
Akizungumzia tukio hilo
Mwenyekiti wa Mtaa wa Bugweto A, Bwana Kulwa Mnyeleshi amesema alipata taarifa
baada ya kupigiwa simu na mmoja wa wanafamilia kwamba Mzazi wao amejinyonga
nyumbani kwake, ambapo alichukua hatua ya kutoa taarifa polisi.
Jeshi la polisi linatoa
wito kwa jamii kuchukua hatua za kuwashirikisha ndugu, jamaa, marafiki au
majirani kutafuta suluhu ya matatizo
yanayowakabili badala ya kuchukua
maamuzi ya kutoa uhai.