LIFAHAMU KIBILA LA WASUKUMA MILA NA DESTURI ZAKE

 


Wasukuma limetokana na neno SUKUMA(KASIKAZINI).Hivyo Msukuma ni mtu wa Kasikazini.
lakini Wasukuma haimaanishi tu watu wa kaskazini bali wanajumuishwa pia watu wa 1.Mashariki(Bhanakiya:Ntuzu):Mkoa wa Simiyu.
2.Kusini(Wadakama,hawa wanaweza kuwa Shinyanga ama Tabora kutegemeana upo wapi). Msukuma wa Mwanza yeye ndio anaona yupo kaskazini hasa kuliko wote kwa hiyo akiwaita watu wa Shinyanga ni wa Kusini(Wadakama) hawezi kuwa amekosea.Japo ukiwa Shinyanga napo utawasikia watu wa Shinyanga wakisema wao wapo kaskazini hivyo ni wasukuma na kusini yao ndio kuna wadakama(Mkoa wa Tabora ndio upo kusini). Inajulikana zaidi kuwa Wenyeji wa Tabora ni Wanyamwezi.Usukumani hakuna kabila la Wanyamwezi bali wanaitwa Wadakama. Japo ukifika Tabora wilaya ya Sikonge na Urambo hasa yenye Wanyamwezi huku wilaya zingine zikiwa kwa kiasi kikubwa zimekaliwa na wasukuma waliotokea Shinyanga na Mwanza miaka mingi iliyopita.
3.Magharibi(Bhanang'weli). Huku utakutana na Wasumva/Wasumbwa. Hawa ndio wanachukua sehemu ya watu wa Magharibi.
Wasumbwa kama ilivyo kwa Wanyamwezi wao wanaonekana kama si sehemu ya Wasukuma lakini ni sehemu ya wasukuma na karibu kila kitu kinafanana kuanzia lugha,mila na desturi na utamaduni wao.
4.Kaskazini(Wasukuma).
Kwa hiyo Wasukuma wamegawanyika katika pande kuu nne za dunia na jina la pande moja ya Kaskazini ndio lililochukua nafasi ya pande zingine zote.
Kabila la wasukuma linapatikana mikoa mitano Mwanza,Geita,Shinyanga,Simiyu na Tabora.
Hii ni mikoa ya Wasukuma. Japo mkoa wa Tabora unajulikana zaidi kama mkoa wa Wanyamwezi na si wasukuma. Japo wanyamwezi asili kabisa ni wachache na wanachukua wilaya ya Sikonge na Mirambo, wilaya zingine zikikaliwa na Wasukuma kuanzia Igunga na Nzega ama mchanganyiko kama Uyui.
hii ni mikoa asili ambayo wasukuma wanatokea.Lakini Wasukuma wengi pia wanapatikana katika mikoa ya Rukwa,Katavi na Morogoro.Ambapo wamehamia huko kwa ajili ya kufata kilimo na malisho ya mifugo.Wasukuma ndio kabila kubwa zaidi nchini Tanzania likifuatiwa na Kabila la Wahaya na baadae Wachagga.

KILIMO NA MIFUGO.
Wasukuma wanafuga kwa wingi ng'ombe,mbuzi na kwa uchache kondoo.
Kwa harakaharaka wasukuma ndio kabila linalofuga ng'ombe wengi zaidi kati ya makabila yanayofuga.mfano sensa ya mwaka 2002 ilionesha kuwa mkoa uliokuwa na ng'ombe wengi zaidi ulikuwa mkoa wa Shinyanga(Shinyanga+Simiyu kwa sasa). Kwa kawaida makabila mengine yote ya wafugaji ukiwatoa wasukuma hakuna kabila lingine ambalo linachukua mkoa mzima. hakuna ubishi kuwa ng'ombe wengi zaidi katika nchi yetu wanamilikiwa na jamii ya wasukuma hasa ukizingatia kuwa mbali na Shinyanga kabla ya kugawanywa bado mkoa wa Mwanza(Mwanza na Geita) na Tabora nayo ilikuwa sehemu ya mikoa ambayo wasukuma wanaishi na kufuga.
Wasukuma pia ni wakulima wa mahindi na mpunga.Zao la biashara Usukumani ni pamba lakini hasa katika wilaya moja ya Maswa iliyopo mkoa wa Simiyu.

MILA NA DESTURI.
Kama ilivyo makabila mengine ya Kiafrika wasukuma wana mila zao na tamaduni zao.Mila za wasukuma zimegawanyika sehemu mbili.

1.Mila za koo ama familia.Hizi hazifanani kabisa kati ya koo na koo.
2.Mila za jumuiya. Hizi zinafana na zinajulikana kwa wanajumuiya/wanachama bila kujali ni wasukuma wa Mwanza,Simiyu(Ntuzu),Tabora(Wanyamwezi),Shinyanga ama wamagharibi(bhanang'weli=wasumbwa).
Jumuiya za mila zipo mbili.

(i)Bhakango,hawa wanafanya kitu kinaitwa bhukango. Mila hizi zinahusu wazazi na watoto wa aina:-
kwanza watoto mapacha. Ukizaa watoto mapacha ni mkosi hivyo lazima ufanye bhukango kuondoa mikosi.wa pili ni watoto waliozaliwa wametanguliza miguu(Kashinje/kashindye). Mtoto akitanguliza miguu kwa maana ya kuzaliwa kinyumenyume huo ni mkosi na lazima ufanye bhukango.Wazazi wa mtoto ama watoto mapacha hupelekwa kufanyiwa matambiko maeneo kama mtoni na huko wao watakuwa uchi kabisa huku wakifanyiwa hayo matambiko na wanajumuiya wenzao.

Katika matambiko haya matusi yote husemwa na ndio lugha rasmi inayotumika hata kama wakiwa njiani wanarudi.Matusi ya kutaja majina viungo vya siri hutamkwa bila aibu yoyote mwanzo mwisho.
Kwa wasioshuhudia siku ukibahatika kukutana nao barabarani wanatukana matusi makubwamakubwa njia nzima wala usishangae.

Kwa kawaida kama si mwanajumuiya wa Bhukango hata ukizaa mapacha ama kashinje mila hii hufanyi.Labda mpaka upate mikosi ama matatizo na uelekezwe na wataalamu wa mila kuwa hao mapacha ama huyo kashinje ndio tatizo basi utalazimika na wewe kuwa mwanachama/mwanajumuiya.
Ili uwe mwanachama sharti uzae mapacha,kashinje,ama wewe ni pacha,ama waliokutangulia ni mapacha mfano ni Shija ambaye huzaliwa baada ya mapacha naye ana sifa ya kuwa mkango.
(ii)Bhasweji, hili ni kundi la pili la wanamila wa kisukuma.

Kundi hili ndio hushughulika na matambiko ya kila aina iwe ni kuondoa mikosi,neema ,nk nk.
Hapa si lazima uwe mwanachama wa moja kwa moja kufanya matambiko haya. Ukipata mikosi,laana nk na njia pekee ni ya kuondoa mikosi hiyo ni matambiko basi hawa mabwana watakuja kukufanyia hata kama si mwanachama.Ila matambiko na ngoma watacheza na kufanyia kwako.

Chakula chao hawali kitu kingine zaidi nyama. Fanya ufanyavyo nyama isikosekane. Kama unapika ugali mboga ni nyama. Kama wali mboga ni nyama.Na wanatabia huwa hawaondoki na wanaweza kukaa kwako hata mwezi wanatambika tu.Usipopika nyama siku hiyohiyo wanaondoka.


WASUKUMA NA NDOA.
Ndoa za kisukuma zinaruhusu ndoa za mitaala(mke zaidi ya mmoja).
Kwa kawaida wasukuma huoa kwa mahali ya ng'ombe kati ya ng'ombe 7 mpaka 20. hii ni kawaida.lakinia mahali inaweza kuwa ng'ombe 25 mpaka 70 kutegemeana na mazingira ya anaeolewa na muoaji.Lakini kubwa kuliko yote ni uzuri na tabia nzuri ya mwanamke.
wasukuma huzaa watoto wengi. Kwa wastani watoto kati ya 6 mpaka 8 ama zaidi na hao ni wa mama mmoja.


WASUKUMA NA WANAWAKE WEUPE.
Ni kweli wasukuma wanapenda wanawake weupe ila weupe natural.
Lakini hili la wanawake weupe si la Wasukuma peke yake bali ukweli ni asimilia kubwa ya wanaume wa makabila yote wanapenda wanawake weupe ila wasukuma ndo wanasingiziwa zaidi utazani wengine hawawapendi wanawake weupe.
CHAKULA CHA WASUKUMA.
Ugali wa mahindi,Ugali wa muhogo na mahindi,Wali,Ugali wa mtama(kipindi cha njaa),maziwa,mboga za kisukuma na nyama. Mboga za kisukuma hasa ni mlenda(rangi=kijani:wakati wa masika),Mkalango(rangi=nyeusi:wakati wa kiangazi) na mzubo(rangi=kijani:wakati wa kiangazi).


NGOMA.
Wasukuma wana aina ya ngoma za burudani zaidi ya 15.
USHAMBA WA WASUKUMA.
Kuna mambo mawili hapa.
1.Wasukuma wana watani wao.
Ushamba wa msukuma umejengwa juu ya watani wa msukuma. Ambapo ni kawaida sana kwa makabila watani wa msukuma kumtania msukuma japo utani unaweza kuwa unabeba sehemu ya ukweli kwa anaetaniwa ila haimaanishi ndo wasukuma wote wapo hivyo.Nje ya makabila watani wa msukuma hata makabila mengine yanatania wasukuma hasa kutokana na ukweli kuwa msukuma kwa kiasi kikubwa hanaga tatizo na jamii yoyote ukiacha wamasai waliokuwa wanatuibia ng'ombe zetu enzi na enzi japo hili sasa ni kama halipo.
2.Maisha ya kijijini. Kama ilivyo makabila mengine wasukuma wengi zaidi wanaishi vijijini na maisha ya vijijini yanafanana kwa karibu makabila yote nchini. kama ni uduni wa mavazi na malazi yanafanana na watu wa vijijini katika jamii zingine,Kama ni kutoyafahamu vyema maisha ya mjini basi ni sawa na watu wa vijijini katika makabila mengine hata kwa watani zetu wagogo.kwa hiyo ieleweke kuwa kila kabila lina washamba na wasio washamba kutegemeana na aina ya ushamba na mazingira ya huyo mshamba.

HAKUNA MAUAJI YANAYOLENGA VIKONGWE BALI KUNA MAUAJI YANAYOLENGA WACHAWI NA ALBINO.
Katika jamii ya wasukuma kama ilivyo jamii zingine kuna wachawi.Swala la wachawi limebakia kuwa swala tete toka enzi na enzi.Utamaduni wa toka zamani kuhusu wachawi ni kuwa ukijulikana ni mchawi uliyeshindikana basi utafukuzwa katika utemi(tawala za kitemizamano)huo na kulazimishwa uvuke temi zingine si chini ya tano. Na ukikaidi unauwawa hadharani na jamii kwa kuwa sehemu kubwa hawapendi uchawi na wachawi. Utamaduni huu wa kuwafukuza wachawi walioshindikana ulikuwa ni wa zamani sana na baadhi ya wachawi walilazimika kuishi kwenye mapango kwa kuwa kila sehemu akienda anakataliwa.

Katika mazingira ya sasa mchawi aliyeshindikana kabisa hafukuzwi kama zamani kwa sababu ya mambo ya sheria bali mtu anaelogwa atajaribu kutafuta dawa za kuzuia uchawi na ikishindikana kabisa basi chaguo la mwisho huwa ni mauaji ambapo atalazimika kukodi watu wa kuua(Kama wahalifu wengine wapo watu wamejiajiri katika uhalifu huu wa kufanya mauaji ya kikatiri kwa hawa wanaodhaniwa ni wachawi).Wanaouwawa huuwawa kwa sababu ya uchawi ila imepotoshwa sana kuwa wanaouwawa ni vikongwe wenye macho mekundu.yapo mauaji mengi yametokea ya watu wasio vikongwe kabisa na wala hawana macho mekundu na pia macho mekundi si ishara ya uchawi usukumani ila imepotoshwa sana na ule wimbo wa kusema ana macho mekundu mleteni hapa ale mapanga.

Mauji ya albino ni jambo ambalo halina taarifa za kina hata kwa wasukuma wenyewe tofauti na mauaji ya wachawi ambayo yanaeleweka kabisa katika jamii ya usukumani.Hakuna taarifa za kueleweka kuhusu jambo hili na huenda ni siri iliyobakia kwa watu wachache miaka mingi.Katika usukumani taarifa za biashara ya viungo vya binadamu zimekuwepo toka zamani lakini zikieleza kuwa biashara za viungo kama ngozi zilikuwa zikiiuzwa kongo kwa ajili ya matumizi ya dawa za kichawi huko.Kuna muda hofu ya wachuna ngozi ilikuwapo kubwa miaka ya 90 na ngozi zilizokuwa zinahusishwa na biashara hiyo ni ngozi za binadamu wa kawaida ambaye si albino.

Swala la albino nalo lilipoibuka taarifa nyingi zilikuwa ni zilezile kuwa viuongo hivyo vina soko kubwa katika nchi ya Kongo. Kuna wakati Kongo iliituhumu Tanzania kuwa biashara ya viungo inafanyika nchini kwetu na wanaouwawa Kongo viungo vinaletwa Tanzania huku na Tanzania pia kuna taarifa kuwa soko ni Kongo.Baadae ikaja kudhihirika kupitia vyombo vyetu vya usalama kuwa waganga wa kienyeji ndio wananunua viungo vya albino. Swala hili bado limebakia kuwa na usiri mkubwa na hakuna taarifa za kueleweka ni nini hasa chanzo chake na soko hili liko wapi?
Ukweli uliowazi ni kuwa mauaji yanatekelezwa na watu wachache waliojivika unyama na kujiajiri katika kazi ya kuua ili wapate kipato chao.

 Na hawa mtandao wao ni mtandao wa kihalifu na si mtandao wa wasukuma Na ndio sababu ikitokea muuaji akajulikana basi anaweza kuuwawa na wanachi wenye hasra kali kwa kuwa hakuna anayependa haya mauaji katika jamii ya usukumani.ukumbuke pia kuwa kanda ya ziwa ndio ina albino wengi zaidi.
UPOLE WA WASUKUMA.

Mwisho kabisa asili ya wasukuma wengi ni wapole,wakarimu na si wachoyo ama wabahiri kama wengi wanvyofikiria pia siyo washamba kama ambavyo wengi wamekuwa wakisambaza picha halisi lakini pia wasukuma huwa na mapenzi ya ukweli akipenda amependa haswa haswa.

Japo haimanishi kuwa hakuna wakali,wachoyo na wabahiri. Nao wapo japo ni wachache sana.
Previous Post Next Post