Na Mapuli Kitina Misalaba
Madiwani wa viti maalum wa Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga wamewakumbusha watendaji, wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika
Halmashauri hiyo kusoma taarifa za mapato na matumizi ili wananchi waweze
kufahamu hatua za maendeleo katika maeneo yao.
Wameyasema hayo leo Ijumaa Julai 12,2024 katika ziara yao kata ya
Nyamalogo na kwamba wameendelea na ziara
yao kwa lengo la kuhamasisha wanawake na wanachama wa CCM na jumuiya zake
kujitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, kuhamasisha
wanawake kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,
Usajili wa wanachama wa CCM na jumuiya zake pamoja na na kukemea Ukatili wa
kijinsia.
Madiwani wa viti maalum Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga wakiongozwa na Mwenyekiti wao Mhe. Zawadi Lufungulo pamoja na mambo
mengine wamewasisitiza watendaji, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kusoma
taarifa za mapato na matumizi katika mikutano ya hadhara kwa kuzingatia
utaratibu uliowekwa.
Wamesema hatua hiyo itawasaidia wananchi kutambua
miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imetekelezwa, inatekelezwa na miradi
inayotarajiwa kutekelezwa katika maeneo yao.
Pia wamesema zoezi la kusoma taarifa za mapato na
matumizi litasaidia kupunguza au kumaliza kabisa kero na malalamiko mbalimbali kwa
wananchi.
Wamesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji
wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kila sekta ikiwemo sekta ya Elimu,
Afya, Maji pamoja na miundombinu ambapo wamesema ni vema kila mwananchi
kuifahamu miradi hiyo kupitia taarifa za watendaji, wenyeviti wa vijiji pamoja
na vitongoji.
Katika hatua nyingine wamaendelea kumpongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali
wananchi wake katika nyanja mbalimbali huku wakiwaomba wananchi kuendelea
kuiunga mkono serikali katika hatua za kuwaletea maendeleo.
Wamempongeza mbunge wa jimbo hilo kwa jitihana mbalimbali
anazozifanya katika kuwaleta maendeleo wakazi wa jimbo hilo ambapo wamesema
yapo mabadiliko makubwa ya maendeleo yamefanyika katika kipindi chake ambayo yalikuwa
ni kero na changamoto kwa wananchi.
Madiwani wa viti maalum hao wamesema badae Mwaka huu
2024 taifa la Tanzania linatarajia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa katika
nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji ambapo
wameendelea kuwasisitiza wanawake kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu ili waweze
kuwatumikia wananchi kwa mujibu wa katiba ya nchi ambayo kwa sasa inatekelezwa kupitia
ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM.
Pia wameendelea kuiomba jamii kuungana pamoja katika
mapambano ya kutokomoza vitendo vya
ukatili vinavyoendelea ikiwemo ubakaji, ulawiti, ndoa za utotoni pamoja na
ushoga unaosababishwa na mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana.
Wametumia nafasi hiyo kuwahimiza wazazi, walezi na
jamii kuwalea watoto katika maadili mema na misingi inayozingatia mila na
desturi za eneo husika ili kuepukana na vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji na
ulawiti unaoendelea kwa watoto.
Kwa upande wake katibu wa umoja wa wanawake UWT Wilaya ya Shinyanga vijijini
Bi. Magdalena Dodoma pamoja na mambo mengine ameendelea kuhamasisha uhai wa
chama ikiwemo wanachama wa CCM na jumuia zake kujisajili katika mfumo wa
kielekroniki.
Pia wamewakumbusha wanawake wa UWT kwenye kata,
matawi na mashina yote Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga vijijini kuhakikisha
wanashiriki katika vikao vyao vya ndani na kwamba hatua hiyo itasaidia
kuwatambua wenye sifa za kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali
za mitaa Mwaka huu 2024 pamoja na uchaguzi mkuu 2025.
Katibu wa umoja
wa wanawake UWT Wilaya ya Shinyanga vijijini Bi. Magdalena Dodoma akiwapa
maelekezo pamoja na faida ya wanachama kujisajili katika mfumo wa kielekroniki kwenye
mkutano wa madiwani wa viti maalum leo Julai 12,2024 katika kata ya Nyamalogo.
Katibu wa umoja
wa wanawake UWT Wilaya ya Shinyanga vijijini Bi. Magdalena Dodoma akiwapa
maelekezo pamoja na faida ya wanachama kujisajili katika mfumo wa kielekroniki kwenye
mkutano wa madiwani wa viti maalum leo Julai 12,2024 katika kata ya Nyamalogo.
Katibu wa umoja
wa wanawake UWT Wilaya ya Shinyanga vijijini Bi. Magdalena Dodoma akiwahimiza
wanawake wa UWT kuwa kipaumbele katika zoezi la uchanguzi wa serikali za mitaa
ikiwemo kuchukua fomu za kugombea.
Katibu wa madiwani viti maalum Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambaye ni diwani wa viti maalum kata ya Tinde Mhe. Anastazia Robart Njile akiwasisitiza wanawake kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali bila uoga na kwamba wajiamini na kumshirikisha mwenyezi Mungu.