MAELFU WANANCHI WAJITOKEZA KATIKA TAMASHA LA SABASABA SANJO YA BUSIYA KISHAPU MKOANI SHINYANGA, MACHIFU ZAIDI YA WATANO, MGENI RASMI KUTOKA KENYA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Tamasha la Sabasaba linalofahamika kwa jina la  Sanjo ya Busiya ambalo linaratibiwa kila Mwaka na ikulu ya Chifu (Mtemi) Makwaiya kwa lengo la kuendeleza mila na desturi katika himaya hiyo iliyopo Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga limehitimishwa Julai 7,2024.

Tamasha hilo hutoa fursa mbalimbali kwa wananchi ikiwemo ngoma za asili pamoja na vyakula vya asili kwa lengo la kuendeleza utamaduni hasa katika kabila la Wasukuma.

Mgeni rasmi katika tamasha la Sabasaba Sanjo ya Busiya Mwaka huu 2024 ni kaunti ya Kitui wa Kabila la Wakamba kutoka nchini Kenya Dkt. Augustus Muli ambaye amewapongeza waandaaji wa tamasha hilo kwa kuendelea kuenzi mila na desturi hasa katika kabila la Wasukuma na kwamba hatua hiyo ni sehemu ya kuwarithisha vijana utamaduni ili wakue katika misingi yenye maadili mema.

Dkt. Muli amesema ni muhimu kuendelea kuenzi mila na desturi za eneo husika ili kuepusha mmomonyoko wa maadili hasa kwa vijana ambapo pia ameipongeza serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono masuala mbalimbali ya utamaduni.

"Tunafurahi kualikwa kwenye tamasha hili la Sanjo ya Busiya na Chief Edward Makwaiya na kuona utamaduni wa Kisukuma, sisi Wakamba na Wasukuma ni ndugu sasa tulioana na majina yetu yanaingiliana, na tutakuja kuwaalika pia mje Kenya,"

"Tunaipongeza pia Serikali ya Tanzania kwa kuunga mkono masuala ya utamaduni, na hapa leo naona viongozi wakubwa wa Serikali akiwamo na Mkuu wa Mkoa, na sisi tutakwenda kufikisha ujumbe kwa Serikali yetu," amesema Chief Dkt. Muli.

Akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema serikali itaendelea kuwaunga mkono viongozi wa kimila ili kuendeleza na kuhifadhi Mila na desturi za mtanzania.

Naye amewapongeza waandaaji wa tamasha hilo huku akiiomba jamii hasa wazazi na walezi kuwarithisha watoto wao mila na desturi zenye manufaa.

"Serikali haina ukabila,lakini ina makabila mbalimbali ambapo wananchi huenzi mila na desturi zao,".

"Nawaomba Machifu mila potofu muziweke kando lakini zile mila nzuri tuzienzi na kuwarithisha vijana ili kuzuia Mmomonyo wa maadili ya vijana," ameongeza Mhe. Macha.

Pia RC Macha ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha viongozi wa kimila kuhamasisha wananchi kwenda kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika badaye Mwaka huu 2024.

Kwa upande wake Mtemi wa himaya ya Busiya Edward Makwaiya ameahidi kuendeleza kushirikiana na serikali katika juhudi za kulinda, kuendeleza na kuhifadhi  Mila na desturi  kwa wakazi wa eneo hilo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo  amepongeza tamasha hilo la utamaduni, kwamba limekuwa na faida sana kwa kuwakutanisha Wasukuma na kuenzi tamaduni zao na kwamba ameahidi kuendelea kuwaunga mkono waandaaji wa tamasha hilo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kufikisha ujumbe kwa wananchi.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria tamasha hilo wameshukuru huku wakiomba kuendelezwa kwa tamasha hilo ambapo wamelitaja kuwa ni fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ya mila na desturi kupitia  elimu inayotolewa hapo.

Tamasha hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, taasisi binafsi, viongozi wa kimila, viongozi wa vyama vya siasa, wadau pamoja na wananchi ambapo wasanii wa ngoma za asili kutoka kabila la Wasukuma na Wakamba wameburudisha katika tamasha hilo.

Baadhi ya viongozi wa kimila waliohudhuria tamasha la Sabasaba Sanjo ya Busiya ni pamoja na katibu mkuu wa umoja wa Machifu Tanzania Chifu Aron Mikomangwa (Nyamilonda wa tatu), Mwenyekiti wa umoja wa machifu Usukumani Chifu Kisendi Joseph Nkingwa (wa pili) kutoka Himaya ya Busumabu Mkoani Mwanza, Chifu Life Nyanono Barisondole wa Himaya ya Karumo Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza, Chifu George Sangija wa Himaya ya Sukuma kutoka Mwanza pamoja na Chifu Charles Dotto Balele kutoka Himaya ya Bujashi iliyopo Magu Mkoani Mwanza.

Himaya ya Busiya ina jumla ya kata kumi (10) na kwamba takribani Miaka kumi na mbili inafanya matamasha hayo ambayo yamejikita katika kuimarisha mila na desturi za wasukuma.







Mgeni rasmi kutoka katika Kabila la Wakamba nchini Kenya Chifu Dkt. Augustus Muli, akiwapongeza waandaaji wa  tamasha la Sabasaba Sanjo ya Busiya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.

TAZAMA VIDEO
Previous Post Next Post