Na Mapuli Kitina Misalaba
Matumizi ya nishati safi ya kupikia yamekuwa njia
muhimu ya kuboresha afya ya jamii katika maeneo mbalimbali, hasa vijijini
ambako kuni na mkaa bado hutegemewa kwa kiasi kikubwa kama vyanzo vya nishati
ya kupikia.
Kupika kwa kutumia kuni au mkaa kuna madhara makubwa
kwa afya kutokana na moshi unaotokana na matumizi ya nishati hizo za asili hata
hivyo, nishati safi kama vile gesi, umeme, na majiko ya kisasa ya kibiashara
yanayoendeshwa kwa teknolojia rafiki kwa mazingira, yameleta mapinduzi ya
kiafya katika familia nyingi.
1. Kupunguza
Magonjwa ya Mfumo wa Hewa
Miongoni mwa athari mbaya zaidi za nishati ya
kiasili ya kupikia ni moshi unaoathiri mfumo wa kupumua ambapo Shirika la Afya
Duniani (WHO) linakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 3.8 hufa kila mwaka
kutokana na magonjwa yanayohusiana na moshi wa kupikia kwa kuni na mkaa.
Magonjwa kama vile pumu, kikohozi sugu, na hata saratani
ya mapafu ni miongoni mwa magonjwa ambayo yamekuwa yakisababisha vifo au matatizo
ya kiafya kwa muda mrefu.
Kwa mfano, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam mwaka 2022 ulionyesha kuwa asilimia 75 ya wanawake vijijini ambao
wanatumia kuni kama chanzo cha nishati ya kupikia, wanasumbuliwa na matatizo ya
kupumua.
Nishati safi kama gesi ya kupikia (LPG), umeme, na
majiko ya kisasa yenye teknolojia rafiki kwa mazingira yameleta mapinduzi
makubwa katika familia nyingi.
Kwa kutumia nishati hizi, wanawake wameweza
kuondokana na magonjwa hayo, na watoto wamepata nafasi ya kukua katika
mazingira yasiyo na hatari ya kiafya.
Ripoti ya mwaka 2023 ya Global Alliance for
Clean Cookstoves ilionyesha kuwa, kwa kutumia nishati safi, viwango vya
magonjwa ya kupumua vinapungua kwa zaidi ya asilimia 40.
2. Kuboresha
Usafi wa Nyumbani
Nishati ya kuni na mkaa si tu kwamba inahatarisha
afya ya mfumo wa kupumua, lakini pia inaathiri usafi wa nyumbani. Nyumba ambazo
zinatumia kuni mara nyingi zinakuwa na kuta zilizochafuka kwa masizi, hali
inayochangia mazingira duni ya usafi hiyo huongeza pia uwezekano wa maambukizi
ya magonjwa ya ngozi na macho. Kwa kutumia nishati safi, mazingira ya ndani ya
nyumba yanakuwa safi zaidi, na watoto wanapata fursa ya kuishi katika mazingira
yasiyo na hatari za kiafya.
3. Kuokoa
Muda na Kuboresha Ufanisi
Wanawake, hasa katika maeneo ya vijijini, wanatumia
muda mwingi kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia. Kazi hii si tu inachosha bali
pia inawanyima muda wa kushiriki katika shughuli nyingine za kiuchumi au za
kimaendeleo kwa kutumia nishati safi kama gesi au umeme, muda wa kupika unakuwa
mfupi, na wanawake wanapata nafasi ya kuwekeza muda wao katika shughuli za
kuzalisha kipato.
Kwa mfano, utafiti uliofanywa na UN Women
katika vijiji vya mkoa wa Shinyanga mwaka 2021 ulionyesha kuwa wanawake
waliotumia majiko ya gesi walipata ongezeko la saa 3 kwa siku ambazo
walizitumia kwenye kilimo na shughuli za kibiashara.
4. Kupunguza
Gharama za Matibabu
Afya bora inayotokana na matumizi ya nishati safi
pia inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za matibabu kwa familia
nyingi. Kupunguza magonjwa ya kupumua kunamaanisha kuwa familia zinapunguza
ziara za hospitalini, na hivyo kuokoa pesa ambazo zingetumika kwa ajili ya
matibabu.
Badala yake, fedha hizo zinaweza kuingizwa katika
mipango mingine ya maendeleo kama vile kulipia ada za shule, au kuboresha
makazi. Takwimu kutoka kwa Tanzania Health Demographic Survey ya mwaka
2022 zinaonyesha kuwa familia zinazotumia nishati safi zinaokoa zaidi ya asilimia
25 ya gharama za matibabu zinazotokana na magonjwa yanayohusiana na moshi wa
kuni.
5. Kusaidia
Mazingira na Kupunguza Mabadiliko ya Tabianchi
Matumizi ya nishati safi pia yana faida kubwa kwa
mazingira. Ukatishaji miti kwa ajili ya kuni na mkaa ni moja ya sababu
zinazochangia ongezeko la gesi joto duniani.
Kwa kupunguza utegemezi wa kuni, jamii inachangia
katika kuhifadhi mazingira. Aidha, matumizi ya nishati safi hupunguza utoaji wa
gesi zinazochafua mazingira, kama vile kaboni dioksidi, hivyo kusaidia
kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi ambapo Serikali ya Tanzania imekuwa
ikiunga mkono matumizi ya nishati safi kupitia sera mbalimbali za kuhamasisha
matumizi ya gesi na majiko ya kisasa.
Hitimisho
Faida za nishati safi ya kupikia ni nyingi na zenye
matokeo chanya kwa jamii na kwamba kupunguza magonjwa ya mfumo wa hewa,
kuboresha usafi wa mazingira ya nyumbani, kuokoa muda, na kupunguza gharama za
matibabu ni miongoni mwa faida zinazosaidia kuinua hali ya maisha ya familia
nyingi.
Kwa hiyo, kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya
kupikia ni muhimu katika kuhakikisha afya bora kwa jamii zetu, na hatimaye,
kuongeza ustawi wa jamii kwa ujumla.