Na Respice Swetu, Kasulu
Wadau wa
elimu katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, wametoa pongezi za
dhati kwa walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kasangezi na shule ya
sekondari ya Muyowozi kutokana na matokeo mazuri ya mtihani wa kuhitimu kidato
cha sita uliofanyika Mei mwaka huu.
Pongezi hizo
zimekuja siku chache baada ya baraza la mtihani la Taifa kutangaza matokeo ya
mtihani huo na kuonesha kuwa, ufaulu wa wanafunzi wa shule mbili za sekondari zenye
kidato cha sita zilizopo katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu, ni wa kiwango
kikubwa.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti bila kutaka kutajwa majina yao wamesema, pamoja na shule
hizo kuwa katika mazingira magumu, walimu na wanafunzi wa shule hizo
wameuthibitishia umma kuwa mshikamano, bidii na uzalendo ni msingi wa
mafanikio.
Wakitoa
mfano wamesema, shule ya sekondari ya Moyowosi iliyoanzishwa mwaka 1913 kwa kutumia
majengo yaliyokuwa kambi ya wakimbizi wa Burundi na Kongo, imekuwa na matokeo
mazuri mwaka hadi mwaka.
Katika
matokeo hayo, watahiniwa 128 kati ya 168 waliofanya mtihani huo kwenye shule ya
sekondari ya Muyowosi wamepata daraja la kwanza, watahiniwa 40 wamepata daraja
la pili, hakuna watahiniwa waliopata daraja la tatu, la nne wala daraja 0.
Kwa upande
wa shule ya sekondari ya Kasangezi iliyoanza kupokea wanafunzi wa kidato cha
tano mwaka 2016, ilikuwa na watahiniwa 222 walifanya mtihani ambapo kati yao 188
wamepata daraja la kwanza, 34 wamepata daraja la la pili, hakuna aliyepata daraja
la tatu, la nne wala daraja 0.
Kutokana na
matokeo hayo, wadau wa elimu katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu wameuomba
uongozi wa halmashauri hiyo kuanzisha shule nyingine za kidato cha tano na sita
ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata fursa hiyo.
“Halmashauri yetu inazo shule mbili
tu za kidato cha tano na cha sita, tunaomba utaratibu ufanyike ili kuongeza
idadi ya shule hizo”,
wamesema.
Katika mkutano
wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Nyakitonto hivi karibuni, mdau mmoja wa
elimu katika kijiji hicho, alimuomba mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Kasulu Dr. Semistatus Mashimba kuipa shule ya sekondari ya Nyakitonto
hadhi hiyo.