Mfanyabiashara maarufu Mjini Njombe, Godfrey Ndambo (45) ambaye ni Mkazi wa Uzunguni Kata ya Ramadhan Wilaya na Mkoa wa Njombe amefariki wakati akipata matibabu mara baada ya kuvamiwa na Majambazi waliompiga na kitu kizito kichwani nje ya geti wakati akiingia nyumbani alipokuwa akitoka kazini kwake na kisha wakaondoka na Tsh. milioni 47 ambazo alitoka nazo dukani kwake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema Mfanyabiashara huyo alivamiwa July 20,2024 saa mbili na nusu usiku wakati akitoka kwenye shughuli zake za biashara ambapo mpaka sasa Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi juu ya tukio.
“Ndambo alivamiwa wakati anatoka kwenye shughuli zake za biashara wakati anaingia getini na kupigwa na kitu kizito kichwani na waliompiga ambao bado hatujajua idadi yao waliweza kutoweka na fedha ambazo zinakadiriwa kuwa ni Tsh. milioni 47 kulingana na taarifa tulizozipata kutoka katika biashara yake ya hesabu zilizofungwa lakini majeruhi alitibwa katika Hospitali yetu ya Kibena na baadaye alihamishiwa Mkoa wa Mbeya na wakati matibabu yanaendelea akafariki”
RPC Banga ametoa wito kwa Wafanyabiashara ambao wamefunga CCTV camera, muda wote ziwe zinafanya kazi ili kusaidia pia katika uchunguzi kwa kuwa kutokana na tukio hilo wamepata changamoto maana camera ndani ya nyumba ya Mfanyabishara huyo hazifanyi kazi kwa kuwa zilikuwa zimezimwa huku pia akiwaomba wanaofanya shughuli za biashara ya fedha kuweka fedha zao benki kuliko kurudi na fedha nyumbani.