MFUKO WA HIFADHI YA JAMII WA PSPF KUTOKA ESWATINI WAFURAHIA MAFANIKIO NSSF

 



*Katambi asema NSSF inazidi kuimarika, unaweza kulipa mafao bila kutetereka

Na MWANDISHI WETU,
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi ameushukuru Ufalme wa Eswatini kuja Tanzania kujifunza mambo mazuri yaliyofanywa na Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambao umekuwa na ustahimilivu wa muda mrefu na unaweza kulipa mafao kwa wanachama wake.

Mhe. Katambi amesema hayo mwishoni mwa wiki katika ofisi za NSSF, Dar es Salaam, wakati akizungumza na ujumbe kutoka Ufalme wa Eswatini ukiongozwa na Mhe. Mabulala Maseko, Waziri wa Utumishi wa Umma, Wabunge na wataalumu kutoka Mfuko wa PSPF chini ya Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Sammy Dlamini.

Ujumbe huo ulifika nchini kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu wa mambo mbalimbali yanayofanywa na NSSF kuanzia mabadiliko ukiwa Mfuko wa akiba NPF mpaka kuwa Mfuko wa NSSF, uwekezaji, ukusanyaji michango na kusajili wanachama.

Mhe. Katambi amesema baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, NSSF imefanikiwa kuendesha shughuli zake kidijitali ambapo sasa wanachama wanaweza kupata taarifa zao mbalimbali kupitia simu ya kiganjani bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF jambo ambalo linawaondoshea usumbufu.

Amesema NSSF pia imepata mafanikio mbalimbali yakiwemo kuwa na ustahimilivu wa muda mrefu na kulipa mafao bila ya kutetereka, umeweka miradi ambayo inatoa huduma kwa wananchi na imekuwa ikizalisha kwa ajili ya kutoa huduma kwa wanachama na namna inavyolipa mafao kwa wanachama wake kwa wakati.

Kwa upande wake, Mhe. Maseko amesema wamefurahishwa na hatua mbalimbali ambazo NSSF imepitia tangu kuanzishwa kwake na jinsi inavyofanya vizuri kwenye mifumo na uwekezaji wake.

“Tuko hapa kujifunza kutoka kwa marafiki zetu na kuona jinsi wanavyoendesha Mfuko wao ambao bado ni endelevu kwa kutoa huduma kwa wanachama na kukusanya mapato yake kwa kutumia mifumo mbalimbali,” amesema Mhe. Maseko.

Amesema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekuwa na manufaa makubwa kwa kupunguza umasikini kwa wananchi, kuleta ustawi wa nchi na ukuaji wa uchumi ambapo inawaweka wananchi katika hali ya usalama kwa kuwa wana uhakika wa kufanya shughuli za maendeleo.

“Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekuwa na ustawi mzuri kwa Tanzania, lakini siyo Tanzania tu, tutafurahi kuona mafanikio haya yakinufaisha Afrika kwa ujumla ili kupunguza umasikini,” amesema Mhe. Maseko.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba amesema ujumbe huo wa Eswatini umefika nchini kwa ajili ya kujifunza na kupata uzoefu kwa mambo mbalimbali kuanzia uandikashaji wa wanachama, ukusanyaji michango, uwekezaji na kulipa mafao pamoja ilivyoweza kutoka kwenye mfumo wa zamani ambao walikuwa wanalipa mafao ya muda mfupi mpaka kutoa mafao ya muda mrefu.

“Sasa hawa wenzetu walitaka kufahamu tulifanya vipi, tulianza kuchukua hatua gani na tulitumia wataalamu gani mpaka tunafika hapa tulipofikia na wamefurahi sana kwa sababu ni kitu ambacho wanaenda kukifanya katika nchi yao,” amesema Bw. Mshomba.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi wa Mfuko wa PSPF wa Eswatini, Bw. Sammy Dlamini, amesema wamejifunza mambo mengi mazuri yaliyofanywa na NSSF tokea ilipoanzishwa mpaka ilipofikia sasa.

Ujumbe huo wa Ufalme wa Eswatini ulikuwa na watu tisa ukiongozwa na Mhe. Mabulala Maseko, Waziri wa Utumishi wa Umma, Wabunge na wataalam kutoka Mfuko wa PSPF chini ya Mwenyekiti wa Bodi, Bw. Sammy Dlamini.



Previous Post Next Post