Mshauri wa Ubora wa Huduma za Afya Mradi wa Afya Hatua THPS Makao Makuu, Agnes Kirato (kulia) akimwelezea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha kuhusu huduma za afya zinazotolewa na THPS.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Asasi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Health Promotion Support
(THPS) imeendelea kutoa elimu na huduma za kupima VVU, afua za kinga, uchunguzi
wa Saratani ya mlango wa kizazi na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwenye maadhimisho ya siku ya Afya Duniani ambayo
katika Mkoa wa Shinyanga yanafanyika
kwenye uwanja wa CCM Kambarage.
Maadhimisho hayo yanafanyika kupitia kampeni ya “Afya yangu, haki
yangu” maarufu AFYA CODE CLINIC SHINYANGA na kwamba yanafanyika kwa siku nne ambapo yatahitimishwa
Jumamosi Julai 27 Mwaka huu 2024.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha pamoja na mambo
mengine leo ametembelea banda la THPS na kupongeza kwa huduma hizo zinazolenga
kutatua changamoto za kiafya kwa wananchi.
"Kwanza niwapongeze kwa kazi kubwa
mnayofanya na sisi tunawashukuru , ni vizuri kuwa na maeneo kama haya kwa maana
ya kwamba tunataka watu wakimbilie kwenye maeneo yanayotoa elimu kwa sababu
elimu ndiyo tiba ya kwanza halafu kupima ni tiba ya pili halafu inayofuata
kushauriwa ya tatu ni matibabu. Kama watu wangetumia muda mwingi kupata elimu
mambo mengi tungeweza kuyaepuka",amesema Mhe. Macha.
"Nimeona THPS mnafanya huduma ya Tohara
Kinga kwa wanaume,Ndugu zangu Tohara Kinga siyo jambo la siri wananchi
jitokezeni kupata tohara Kinga",amesema Mhe. Macha.
Kupitia mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa
Rais wa Marekani wa kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia kituo cha kudhibiti
na kuzuia Magonjwa cha Marekani ( CDC), Tanzania Health Promotion Support
(THPS) inashiriki katika maadhimisho hayo kwa kutoa elimu na huduma za Afya kwa
wakazi wa Shinyanga.
Meneja mradi wa THPS Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Amos Scott ametumia
nafasi hiyo kutaja mafanikio ya asasi hiyo ambapo amesema kwa kipindi cha Mwezi
Oktoba 2023 hadi Juni 2024 jumla ya wapokea huduma 21,759 walipimwa Saratani ya
mlango wa kizazi ambapo 563 waligundulika kuwa na viashiria vya Saratani hiyo
na 552 kati yao walipatiwa matibabu.
“Tunaendelea kuwaokoa akina mama dhidi ya
saratani ya mlango wa kizazi, Tunaomba wanawake wajenge tabia ya kupima afya
zao kwani saratani nyingi zikiweza kufanyiwa uchunguzi wa awali zinatibika, isipotibiwa
mapema ni ngumu kutibiwa”,amesema Dkt. Scott.
DKT. Scott amesema THPS imeendelea kutoa huduma za Afya mahususi
kwa vijana na kwamba hadi kufikia mwishoni mwa Mwezi Juni 2024, mradi wa Afya
Hatua umetoa huduma kwa vijana 4,027 wanaoishi na VVU ambapo 3,082 ni wanawake
na 1,125 na wanaume huku akieleza kuwa THPS inafanya kazi na vituo mbalimbali
vya kutolea huduma za Afya ili kuhakikisha matumizi sahihi ya dawa za kufubaza
VVU kwa wapokea huduma.
THPS inafanya kazi kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania
kupitia Wizara za Afya za Tanzania Bara na Zanzibar; Wizara ya jinsia, vijana,
wazee, na makundi maalum; ofisi ya Rais, tawala za Mikoa na serikali za mitaa
na Wizara ya mambo ya ndani ya nchi.
Kwa ufadhili wa mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa Misaada
ya UKIMWI (PEPFAR) kupitia kituo cha kudhibiti na kuzuia Magonjwa (U.S. CDC),
THPS inatekeleza afua mbalimbali za VVU\UKIMWI; kifua kikuu; kuzuia ukatili wa
kijinsia dhidi ya watoto; huduma za Afya ya uzazi, watoto wachanga, watoto na
vijana; mifumo ya habari ya maabara na usimamizi wa Afya na UVIKO – 19.
Aidha kuhusu mradi wa CDC\PEPFAR Afya Hatua (Oktoba, 2021 –
Septemba, 2026) mradi huo unalenga kutoa huduma jumuishi katika vituo vya Afya
ukiwemo Mkoa wa Kigoma, Pwani, Shinyanga na Tanga.
Pia huduma hizo ni pamoja na matibabu na matunzo ya watu wanaoishi
na VVU, huduma za kitabibu za tohara kwa wanaume katika Mikoa ya Kigoma na
Shinyanga na program ya DREAMS kwa wanawake katika Mkoa wa Shinyanga.
Wakizungumza baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga wameishukuru asasi ya THPS kwa huduma nzuri na kwamba zimesababisha kufahamu hali zao za kiafya huku wakiahidi kuzingatia maelekezo waliyopewa kwa lengo la kuimarisha Afya zao.
Meneja mradi wa THPS Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Amos Scott akizungumza
katika maadhimisho hay oleo Alhamis Julai 25,2024.
Meneja mradi wa THPS Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Amos Scott akizungumza
katika maadhimisho hay oleo Alhamis Julai 25,2024.
Mshauri wa Ubora wa Huduma za Afya Mradi wa Afya
Hatua THPS Makao Makuu, Agnes Kirato (kulia) akimwelezea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.
Anamringi Macha kuhusu huduma za afya zinazotolewa na THPS
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha akiwapongeza watumishi wa THPS kwa kuendelea kutoa huduma rafiki kwa vijana ikiwemo upimaji wa VVU, uchunguzi wa magonjwa ya ngono, utoaji wa dawa Kinga (PrEP), uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza na uchunguzi wa kifua kikuu.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.
Anamringi Macha akiwapongeza watumishi wa
THPS kwa kuendelea kutoa huduma rafiki kwa vijana ikiwemo upimaji wa
VVU, uchunguzi wa magonjwa ya ngono, utoaji wa dawa Kinga (PrEP), uchunguzi wa
magonjwa yasiyoambukiza na uchunguzi wa kifua kikuu.