MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM),Mkoa wa Geita Manjale Magambo amewataka wanachama wa chama hicho kutokuruhusu watu kuwagawa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Manjale amesema hayo wakati wa shughuli ya kupandisha bendera za Chama kwa mabalozi ambao wapo kwenye mtaa wa Kivukoni kata ya Kalangalala Wilayani Geita.Zoezi ambalo limeambatana na harambee ya ujenzi wa ofisi za Chama tawi la Kivukoni.
Amesema wanapoelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa,vijiji na vitongoji pamoja na ule mkuu wa mwaka 2025 wanachama wanatakiwa kuwa wamoja na kuwapuuza watu ambao wamekuwa wakija kwa nia ya kutaka kuwagawa na kutumia vibaya jina la Rais Samia Suluhu Hassan.
“Kuna watu wanakuja wakidai wametumwa na Rais Samia Suluhu Hassan,sidhani kama Rais anauwezo wa kutuma mtu wakati yeye shughuli zake zinajieleza najua kuna wahuni ambao wamekuwa wakija na maneno matamu lakini sisi tumesema tutadili na wahuni wote hatutakubali kuona watu wanamchafua Rais wetu na sisi tukae kimya”Alisema Manjale Magombo.
Aidha Manjale amesema ni vyema kwa wananchi wakajitokeza kwa Wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na wawe tayari kwenda kuchagua viongozi sahihi na kwamba chama hakipo tayari kuwabeba watu ambao awakufanya vizuri wakati walipopewa madaraka ya kuwatumikia wananchi.
Sanjali na hayo Manjale amechangia kadi za chama elfu mbili pamoja na kiasi cha Sh,Milioni 3 ambazo zitatumika kununua eneo la kujenga ofisi za chama tawi la Kivukoni.“Mwenyekiti wetu wa Taifa tulipokaa naye alisema ni vyema twende tukawe na ofisi kuanzia kwenye matawi,Kata ,Wilaya hadi Mkoa pamoja na vitega uchumi na mimi nataka niungane na wana kivukoni katika kufanikisha malengo ya ujenzi wa ofisi sipendi maneno na ahadi natoa Milioni 3 za ununuzi wa kiwanja sasa tuanze kutafuta pesa za mawe,tofari pamoja na saruji”Alisema Manjale Magambo.