Adeladius Makwega-MWANZA
Tangu mwaka 2016 mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Marehemu Rais John Pombe Magufuli na baada ya kifo chake yaani mwaka 2021 Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan kumekuwa desturi nzuri na ya kiungwana kwa Serikali kufanyia kazi malalamiko dhidi ya viongozi wanaolalamikiwa, kwa kupisha uchunguzi na zoezi la utenguzi kufanyika hasa katika mambo yanayogusa maslahi ya umma.
Aya hiyo juu haina maana kuwa serikali za awamu zilizotangulia yaani awamu ya 1, 2, 3 na 4 ziliyafumbia macho malalamiko ya wananchi dhidi ya viongozi walipoonekana kukengeuka.
Mfano thabiti ni Serikali ya Awamu ya Nne ya ndugu Jakaya Kikwete ambapo ilitengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya Bukoba aliyewacharaza viboko walimu mhe. Albart Mnali kitendo hicho kilionekana siyo cha heshima, si cha kiungwana na kitendo cha kikoloni maana hata kama walimu wana makosa mamlaka zao za nidhamu zilikuwepo. Kikubwa msomaji wangu maamuzi yalifanyika yanafanyika na yanapaswa kuendelea kufanyika kama kuna jambo linaolalamikiwa dhidi ya mhusika yoyote ambaye ni kiongozi wa umma na ana tuhuma za kukengeuka hadharani na maamuzi hayapashwi kuchelewa. Kwa hakika Serikali ya Awamu ya Sita ilifanya maamuzi ya utenguzi wa viongozi wa wawili kwanza Bi Pauline Gekul ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria kwa tuhuma za kumdhalilisha kijana wa kiume na pili ilifanya utenguzi wa hivi karibuni wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Yahaya Ismairl Nawanda kwa tuhumu za kumlaiti binti mmoja mkoani Mwanza ambapo shauri hilo lipo mahakamani linaendelea kusikilizwa.
Kwa hakika jamii ya Watanzania hivi karibuni imeshuhudia Waziri Nape Nnauye anayeshugulikia masuala ya Habari na Tekinolojia ya Habari akinadi hadharani juu ya namna ya kushinda uchaguzi kwa bao la mkono.Kichwani kwake akiwa amevalia kofia ya chama chetu cha CCM huku kiwiliwil chake kikiwa kimebeba uwaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndugu yetu Nape Nnauye vipi? Mbona unatupeleka machakani ?Mbona unakengeuka ?
Katika taarifa zilizohifadhiwa hadi katika vyombo vya habari kwa maandishi , sauti na video kuna malalamiko mengi yawe ya upinzani jimboni kwa Nape Nnauye (Rejea Mchezaji wa zamani wa soka na mpinzani wa Nape Seleiman Mathew na malalamiko ndani ya CCM yenyewe dhidi ya huyu huyu Nape Nnauye.
“Nape ni nani?Ngoja Niwaambie Watanzania, Tusidanganyane hapa, Ndugu Kinana ni miongoni mwa watu ninaowaheshimu lakini nilianza kutilia mashaka urafiki wa Nape na Kinana siku wabunge wa CCM tunawapigia kura wabunge wa Afrika Mashariki. Nape Mwenezi; Kinana Katibu Mkuu.Katika kura kulikuwa na ushindani mkubwa na wagombea waliokuwa Very Strong. Kwa upande wa akinamama wakachuana wanawake, Tulipopiga kura tu Nape akaingia chumba cha kuhesabu kura. Kwa bahati mbaya katika wagombea kukawa na mkwewe Nape anaitwa mama Mkami.Nape akawa anahesabu kura kila akishika kura anataja mama Mkami. Mpaka tunamaliza uchaguzi(kuhesabu) mama Mkami wa kwanza. Hapo hapo mgombea mmoja anaitwa Angela Kiziga akalalamika, naye shy -Rose Bhanji akalalamika, haiwezekani huyu mtu awe wa kwanza hakuna anayemjua, haiwezekani awe wa kwanza, amepataje hizo kura? Ndugu Kinana alipoona joto kali akaniita mimi(Lusinde), Martha Mlata na Mhinde Tambwe akasema rudieni kuhesabu hizo kura, akasema nataka nione kama kuna mabadiliko na ubadhilifu.Tumerudia kuhesabu mama Mkami hata 20 bora hayupo! Hata 20 bora hakuwepo.Tumerudia kuhesabu wa kwanza akawa Angela Kiziga ambaye Nape alikua amemuibia kura zake na mimi nilitegemea ndugu Kinana angechukua hatua ya kumuwajibisha Nape lakini hadi tunaondoka pale Karimjeee Kinana Katibu Mkuu Nape Mwenezi.”
Haya ni maelezo ya kina yanayoonesha tabia ya Nape Nnauye katika chaguzi na si maelezo ya Seleiman Mathew bali ni maelezo ya mwana CCM mh. Livingstone Lusinde akiwa pia Mjumbe wa Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa. Kibaya maelezo haya hayajawahi kukanushwa hata siku moja.Haya yote ni mambo ya Nape Nnauye, kwa hakika ni jambo la kushangaza mno ambapo Mwanakwetu anayatafakari na tafakari hiyo inambeba hadi katika tukio moja la kweli la miaka mingi nyuma ambapo Mwanakwetu akiwa na miaka 10 na ushehe.
“Mwaka 1987 nilitoka Mbagala na Padri Fidelis kwenda Kanisa la Mtakatifu Fransisko Ksaveri–Chang’ombe pale Machinjioni jirani na Kituo cha Polisi Chang’ombe, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam- kando ya makutano ya Barabara(mataa) jirani na Shule ya sekondari Kibasila. Paroko wa Chang’ombe Padri Deogratias Mbiku ambaye baadaye alikuwa Monsinyori ambaye alikuwa na mguu mmoja mfupi mwingne mrefu alimuomba Padri Fidelis akasalishe misa ya mazishi, siku hiyo mosinyori hakuwepo Parokiani.
Nakumbuka mawasiliano yalifanyika kwa simu za kizamani. Katika gari la Padri Fidelis Gofu rangi ya udongo nilikuwamo mimi, Benson Masonoro na Padri Fidelis mwenyewe tukafika Chang’ombe tukainga sakalistia Padri akavaa nguo za misa na mimi na Masonoro tukavaa kanzu za watumikiaji na Padri akasalisha misa hiyo ya mazishi.
Nyimbo za misa ile zilizoimbwa zilifahamika na watu wengi na huku nyimbo hizo kinanda kikiongoza vizuri. Kabla ya misa kuanza niliona watu wanahangaikanamna ya kukiwasha kinada hicho huku wakikivua nguo iliyofunika kinanda. Nyimbo hizo ziliimbwa vizuri kianda kikisindikiza misa yote ya mazishi. Misa ilipokwisha wakati tunakwenda makaburini Chang’ombe Padri Fidelis alifurahishwa mno na jamaa aliyepiga kinanda. Akauliza ni nani aliyepiga kinanda hicho? Akaitwa pale tulipo akatumbulishwa huyu ndiye Moses Nnauye, Padri Fidelis alifurahi mno kwa ndugu Mnauye alivyoshiriki misa hiyo huku akijua kucheza kinanda kwa nyimbo ambazo nota zake hazikuwepo na wala hawakujiandaa na hata imani yake pengine haikuwa Ukristo. Baada ya mazishi tukarudi zetu Mbagala.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika mtu yoyote ambaye anajinasibu kuwa ni hodari wa wizi wa kura mtu huyo hafai kuwa kiongozi wa umma maana kauli hiyo inafanya jamii kutomuamini na hata kuleta migogoro ya uchaguzi na viongozi wengine hawapaswi kumuamini pia . Kauli tata kama hizo zinafanya jamii kutokuwaamini viongozi walioshinda chaguzi zilizopita na hali hiyo inajenga kutokuziamini tume za uchaguzi zilizopita na hata zijazo na pia hata wale waliyoziongoza na wengi wao ni majaji wastaafu. Mwanakwetu anaipongeza CCM kwa kujitenga na kauli hiyo lakini hilo halitoshi lazima CCM imuadhibu zaidi Nape Nnauye.
Rais wa awamu ya sita Mh Samia Suluhu Hassan arejea utenguzi wa Albart Mnali, akumbuke na arejee utenguzi wa Pauline Gekul na hata utenguzi wa Yahaya Isimairi Nawanda . Hapa Nape Nnauye amenajisi kura zinazopingwa na Watanzania na anachafua chaguzi zote zinazofanyika kila baada ya miaka mitano.
Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kujitenga a kauli hiyo. Nape Mnauye mwenyewe anawajibu wa kutambua anabeba jina la Brigedia Mosea Nnayue ambaye alikuwa kiongozi mzuri, mwenye heshima, muungwana kwa watu wote na imani zao za dini rejea kisa kile cha kupiga kinanda Katika Kanisa la Mtakatifu Fransisko Kizaveli Parokia ya Chang’ombe Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Mwanakwetu Upo? Kumbuka,
“Nape ni nani? Ngoja Niwaambie Watanzania Ukweli, Tusidangnayane.”.
Nakutakia Sku Njema.