PROF. SHEMDOE: MAAZIMIO YA MKUTANO WA KIMATAIFA WA SAYANSI WA TAASISI YA NELSON MANDELA YAWEKWE KATIKA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050

 


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akiongea na washiriki wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Upeo wa Kitropiki Uendelevu wa kilimo, mazingira na teknolojia ulioandaliwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Julai 17,2024 katika Hoteli ya Mount Meru Arusha.
  

Washiriki Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Upeo wa Kitropiki Uendelevu wa kilimo, mazingira na teknolojia ulioandaliwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ambao ni Watafiti na Wanataaluma wa masuala ya kilimo,mazingira na teknolojia wakimsikiliza mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Julai 17,2024 katika Hoteli ya Mount Meru Arusha.

   

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe(Katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Upeo wa Kitropiki Uendelevu wa kilimo, mazingira na teknolojia ulioandaliwa na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.

.......

Na.Mwandishi Wetu _Arusha

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amewataka washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Sayansi wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela wenye kauli mbiu ya Uendelevu wa kilimo, mazingira na teknolojia kuhakikisha maazimio ya mkutano huo yanaingia katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuleta matokeo chanya katika kilimo, mazingira na teknolojia nchini.

Prof. Shemdoe ameyasema hayo Julai 17, 2024 wakati akifungua mkutano huo wa siku tatu katika Hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, uliowakutanisha wadau na wataalamu wa sekta hizo kutoka ndani na nje ya nchi, lengo ikiwa ni kujadili matokeo ya tafiti za kilimo, mazingira na teknolojia ili kuendeleza sekta hizo.

“Kupitia maazimio ya mkutano huu wa kujadili matokeo ya tafiti zilizofanyika yatasaidi na kuwawezesha watunga sera, kutunga sera zenye kuleta mabadiliko kwa ajili kuleta maendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja na kukuza uchumi wa nchi” amesema Prof. Shemdoe.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi upande wa Taaluma, Utafiti na Ubunifu Prof. Anthony Mshandete kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Taasisi ameeleza kuwa, maazimio ya mkutano huo yatagusa nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda, wakulima na wadau wa mazingira ili kutoka na andiko litakalotoa mchango wa namna ya kuendeleza kilimo, utunzaji mazingira na matumizi ya teknolojia katika dira ya taifa ya 2050 ili kuvirithisha vizazi vijavyo.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo ambaye ni Profesa Mshiriki katika Taasisi hiyo Prof. Linus Munishi ameeleza kuwa, mkutano huo ni wa kwanza kufanyika, lengo ikiwa ni kutoa matokeo ya utafiti kutoka kwa wataalamu kwa ajili ya wadau ili kuweza kutatua changamoto zitokanazo na maendeleo ya kijamii, kiuchumi na utunzaji wa mazingira.

Mkutano wa Kimataifa wa Sayansi wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela umefanyika kwa mara ya kwanza ukihusisha wadau wa sekta mbalimbali za kitaaluma kwa kushirikisha wadau wa kilimo, mazingira na teknolojia ili kwa pamoja kuweza kuunganisha matokeo ya kiutafiti kwa kuyaweka katika machapisho yatakayosomwa na wadau wa maendeleo katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Previous Post Next Post