RAIS SAMIA KULIPIA GHARAMA ZOTE ZA MATIBABU KWA MTOTO ALIYEKATWA SHINGONI NA KUTENGANISHWA NJIA YA HEWA GOBA

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan atalipia gharama zote za matibabu kwa mtoto Maliki Hashimu (5) mkazi wa Goba Jijini Dar es Salaam, anayetibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na majeraha makubwa aliyopata baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni kilichotenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti hivyo kusababisha ashindwe kupumua, kuongea, kupata maumivu na kupoteza damu nyingi sana.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) mapema leo alipotembelea Hospitali hiyo.

Hospitali ya Taifa Muhimbili, kupitia watalaam wake tayari wamemfanyia upasuaji mkubwa mtoto huyo ambao ulichukua muda wa saa nne ili kurekebisha njia ya hewa, sanduku la sauti, matezi yaliyopata changamoto kwenye shingo na kutibu jereha la nyuma ya shingo.

Waziri Ummy amewapongeza watoa huduma wote kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuhudumia wananchi kwa weledi.

Jeraha la mbele ya shingo, liliharibu tezi la mbele liitwalo (thyroid gland) kwa kulikata katikati na kusababisha mtoto huyo kuvuja damu kwa wingi, kupata maumivu makali kutokana na jeraha alilokatwa mbele ya shingo sehemu iitwayo (trachea) ambako hewa inayotoka kwenye mapafu hupita ili iweze kwenda kwenye sanduku la sauti kumuwezesha kuhema na kuongea kwa mantiki.

Hospitali ya Taifa Muhimbili ilimpokea mtoto huyo usiku wa kuamkia jumatatu wiki hii na kwa sasa yupo chini ya uangalizi maalum akiendelea kupata matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali hiyo.

Previous Post Next Post