Na Lucas Raphael,Tabora
SERIKALI imevitaka Vyama vya Ushirika vilivyopo maeneo ya vijijini kuendelea kuomba uwakala wa kusambaza pembejeo za kilimo ili kuboresha usambazaji wake kwa wakulima.
Hayo yamebainishwa jana na Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde alipokuwa akifungua Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Fatuma Mwasa Ipuli Mkoani hapa.
Alisema kuwa kutokana na vyama vya ushirika kufanya vizuri katika eneo hilo la usambazaji pembejeo ikiwemo kufika kwa wakati serikali inavishauri kuendelea kuomba ili kuwarahisishia wakulima.
Aidha Naibu Waziri aliitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na wadau wengine kuhamasisha uanzishwaji wa Vyama vya Ushirika katika sekta nyingine za kiuchumi ili kuwafikia wanachi wengi zaidi.
Alieleza kuwa hili litasaidia kuongeza wanachama wa Vyama vya Ushirika kwani zaidi ya aslimia 84 ya Vyama vya Ushirika vipo katika sekta za Kilimo na Fedha huku akibainisha dhamira ya serikali kuwa ni kuwafikia wananchi wengi zaidi.
‘Nawapongezeni kwa mafanikio makubwa yaliyopata sasa katika sekta hizi mbili (Kilimo na Fedha) lakini mwamko wa kuhamasisha maendeleo ya ushirika kwenye sekta nyingine bado ni mdogo sana’, alisema.
Naibu Waziri alifafanua kuwa vyama vya ushirika vina manufaa makubwa kwa wananchi hivyo akatoa msisitizo kwa Tume kufanya kila linalowezekana ili kuongeza Vyama vya Ushirika na wanachama ikiwemo kuimarishwa ushirika.
Alibainisha kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Tanzania Bara kuna watu mil 59.8 kati yao mil 20.6 sawa na asilimia 34 wanaishi Mjini na mil 39.2 sawa na asilimia 66 wanaishi vijijini.
Aidha alifafanua kuwa idadi ya kaya kwa nchi nzima ni mil 14.3 huku vijijini zikiwa ni mil 8.6,hali hiyo inayoonesha kwamba katika kila kaya 2 kaya 1 inanufaika na ushirika (ina mwanachama wa ushirika).
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo inaonesha hakuna Mtanzania ambaye hanufaiki na ushirika, hata kama sio yeye basi mmoja wapo katika familia au ndugu ananufaika na ushirika.
Naibu Waziri aliahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Tume ya Maendeleo ya Ushirika itahakikisha ushirika unaimarishwa zaidi ili Watanzania wengi wanufaike.