SHEIKH WA MKOA WA SHINYANGA KUPOKEA MAADAMANO YA MAADHIMISHO YA MWAKA MPYA WA KIISLAM

Waumini wa Dini ya Kiislamu katika mkoa wa Shinyanga, kesho Jumamosi tarehe 13.07.2024, wataungana na Waislamu wenzao kote duniani kuadhimisha mwaka mpya wa kiislam 1,446.
Akizungumza kwa niaba ya Sheikh mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mjumbe wa baraza la washauri wa Sheikh Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sheikh Masoud Kanyuguta, amesema maadhimisho hayo yataanza saa 10:00 jioni kwa maandamano yatakayoanzia katika Msikiti wa Quba uliopo kona ya Buhangija mjini Shinyanga ambayo yataelekea mpaka kwenye Makaburi ya Kitangili kwa ajili ya dua kwa watu waliotangulia mbele za haki.
Sheikh Kanyuguta ambaye pia ni Sheikh wa Kata ya Hemed bin Jumaa bin Hemed, amesema maandamano hayo yatahitimishwa katika Msikiti wa Taqwa uliopo Kizumbi nje kidogo ya mji wa Shinyanga na yatapokelewa na Sheikh mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ismail Habib Makusanya.
Keshokutwa Jumapili tarehe 14.07.2024, maadhimisho hayo yataendelea kwa michezo mbalimbali ikiwemo Mpira wa miguu kati ya Maimamu na Makatibu wa Misikiti yote ya Kata ya Mufti Hemed Bin Jumaa Bin Hemed, kukimbiza kuku kwa wanaume na wanawake wa kuanzia umri wa miaka 55, kuvuta Kamba kwa wanaume na wanawake, Mashindano ya kukimbilia Kanga itakayowekwa Mita 100 kwa wanawake wa umri wa miaka zaidi ya 20 hadi 30 na miaka zaidi ya 50 pamoja na michezo ya watoto.
Mgeni rasmi katika michezo hiyo ambayo itafanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Kitangili kuanzia saa 10:00 jioni, atakuwa Sheikh Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Sheikh Ismail Habib Makusanya ambaye atafungua kwa kupiga Pernati itakayodakwa na Sheikh mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Sheikh Soud Suleiman Kategile.

Sheikh Kanyunguta amewaomba Waislam wote na wasio Waislam kushiriki matukio yote ambayo yatafanyika kuanzia siku ya kwanza ya maadhimisho na kilele chake siku inayofuata. 

Previous Post Next Post