SHIRIKA LA WAMATA LAZINDULIWA RASMI MKOANI SHINYANGA

Mwenyekiti wa shirika la WAMATA Taifa Bwana Lekoko Ngitiri akizungumza kwenye uzinduzi wa shirika hilo Mkoa wa Shinyanga.


Na Mapuli Kitina Misalaba

Shirika la Wateule wa Mama Tanzania (WAMATA)  Ijumaa Julai 5,2024 limezinduliwa rasmi Mkoani Shinyanga kwa lengo la kuisaidia serikali katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kijamii na kisiasa.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali na kwamba umekwenda sanjari na maadamano ya amani kupita maeneo mbalimbnali ya Manispaa ya Shinyanga.

Mwenyekiti wa WAMATA Taifa Bwana Lekoko Ngitiri amewasisitiza viongozi wa shirika hilo Mkoa wa Shinyanga kushirikiana na serikali katika utatuzi wa changamoto na kero zinazowakabili wananchi.

Amewahimiza kuendelea kuisemea serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye jamii ili wananchi waendelee kuunga mkono jitihada za serikali.

Bwana Ngitiri pia amewasisitiza viongozi hao wa shirika la WAMATA kuendelee kukiunga mkono Chama cha Mapinduzi CCM na kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa Mwaka huu 2024 pamoja na uchaguzi mkuu 2025 chama hicho kinapata viongozi wawakilishi bora katika kata na majimbo yote ya uchaguzi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirika la WAMATA Mkoa wa Shinyanga Bi. Sophia Emmanuel Bujiku ameahidi kusimamia mipango yote ya shirika hilo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Baadhi ya viongozi wengine kutoka Wilaya za Kishapu, Kahama pamoja na Wilaya ya Shinyanga wameahidi kuwa mabalozi wazuri katika kuisemea serikali mazuri yanayofanyika kwenye jamii.

Aidha katibu wa itikadi, siasa na uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Bwana Richard Masele ametumia nafasi hiyo kulipongeza shirika kwa ubunifu wa kuisaidia serikali katika masuala mbalimbali ikiwemo ya kijamii na kisiasa.

Pia katibu mwenezi huyo amezungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa Mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu Mwaka 2025 ambapo amewasisitiza viongozi na wanachama wa shirika la WAMATA kwenda kuwabaini watu wenye ushawishi waweze kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia kupitia Chama cha Mapinduzi CCM.

Maandamano ya amani ya Shirika la Wateule wa Mama Tanzania (WAMATA) ambapo viongozi kutoka Halmashauri na Wilaya zote za Mkoa wa Shinyanga wameshiriki kupita mitaa mbalimbali ya Manispaa ya Shinyanga leo Julai 5,2024. 



 

Previous Post Next Post