Na Lucas Raphale,Tabora
MRADI wa Pamoja wa Wakulima wa Tumbaku (TCJE) umepongeza kazi nzuri inayofanywa na Vyama Vya Ushirika ikiwemo kuhamasisha wakulima kuzingatia elimu ya kilimo bora chenye tija ili kuongeza uzalishaji.
Hayo yamebainishwa jana na Meneja Shughuli wa Mradi huo Goodluck Tairo alipokuwa akiongea na Waandishi wa Habari waliotembelea Banda la Mradi huo kwenye Maonesho ya siku ya Ushirika Duniani yanayofanyika Mkoani Tabora.
Alisema kuwa elimu inayotolewa na usimamizi mzuri wa shughuli za wakulima vimeendelea kuwa chachu kubwa ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo kila mwaka hali inayopelekea wakulima kupata mafanikio makubwa na kuinuka kiuchumi.
Alisisitiza kuwa TCJE kama chombo kinachounganisha wakulima wa tumbaku hapa nchini kinaridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Viongozi wa Union zote na kitaendelea kuhakikisha shughuli za wakulima zinaleta tija kubwa zaidi.
Tairo alibainisha kuwa soko la tumbaku limeendelea kuboreshwa kila mwaka kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya 6 ikiwemo kuhamasisha makampuni mengi zaidi kujitokeza kununua tumbaku ya wakulima.
‘Tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujali wakulima na kuendelea kuboresha sekta ya kilimo nchini ikiwemo kutoa mbolea ya ruzuku kwa wakulima wote, hili ni jambo la kujivunia sana katika nchi yetu’, alisema.
Aliongeza kuwa msimu huu soko limeenda vizuri sana na wakulima walio wengi wameshalipwa fedha zao ila akatoa wito kwa makampuni ambayo hayajakamilisha malipo kuhakikisha wanalipa kwa wakati kabla ya kuchukuliwa hatua.
Tairo alisisitiza kuwa msimu ujao TCJE itahakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati na haitamfumbia macho msambazaji yeyote atakayekwamisha au kufanya udanganyifu wowote ikiwemo kuuza bei tofauti.
Alifafanua majukumu makuu ya Taasisi hiyo kuwa ni kusambaza pembejeo kwa wakulima, kusimamia masoko ya zao hilo hadi sasa kuna makampuni 11 yanayonunua tumbaku, kutoa elimu ya kilimo bora na kuunganisha wakulima.
Aliongeza kuwa Mradi huo ulioanza mwaka 2016 hadi sasa una wanachama 8 ambao ni vyama vya ushirika (Union) kutoka Mikoa 7 na vyama vya msingi (Amcos) 716.
Vyama hivyo ni WETCU 2018 LTD, MILAMBO, KACU, KTCU, SEAMCU, MBCU, CHUTCU na LATCU.