Na Gideon Gregory Dodoma.
Imeelezwa kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwasasa imeongeza kasi ya ushughulikiaji wa malalamiko ya uvunjwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kutokana na upatikanaji wa rasilimali fedha kwaajili ya uchunguzi ambapo kwa mwaka 2022/23 tume hiyo ilikuwa ikishughulikia jumla ya malalamiko 1524 ambapo ilihitimisha jumla ya malalamiko 789 na kufanya malalamiko yaliyoendelea kuanzia Julai 1, 2023 kuwa 885.
Hayo yamebainishwa leo Julai 19,2024 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu ripoti mbalimbali za chunguzi zilizofanywa na Tume kwa Mwaka wa 2023/24.
“Aidha katika kioindi cha kuanzia Julai 10,2023 hadi Mei 30,2024 THBUB ilipokea malalamiko mapya 135 na kufanya malalamiko yanayoshughulikuwa mwaka huo kuwa malalamiko 1020 ambapo katika katika kipindi husika THBUB ilifanikiwa kukamilisha na kuhitimisha uchunguzi wa malalamiko 236 na hivyo uchunguzi wa malalamiko 784 unaendelea “,amesema.
Ameongeza kuwa katika malalamiko hayo, malalamiko 22 yaliilazimu THBUB kufanya uchunguzi maalum huku chunguzi hizo zikihusu masuala ya ardhi, uharibifu wa mazingira, tuhuma za vitendo vya ukatili katika vizuizi na matumizi mabaya ya madaraka.
Sanjari na hayo Jaji Mstaafu Mwaimu amesema miongoni mwa chunguzi zilizofanyika ni tuhuma dhidi ya Jeshi la polisi ambapo tume ilithibitisha kutozingatiwa kwa taratibu za kisheria za ukamataji na ushikiliwaji wa watuhumiwa katika mahabusu ya polisi.
“Vitendo hivyo viliambatana na wananchi kupigwa, kufanyiwa ukatili na mateso na kusababishia majeraha mfano katika lalamiko la mwananchi kutoka Manispaa ya Morogoro, THBUB ilijiridhisha kuwa mwananchi huyo alipigwa na kufanyiwa vitendo vya ukatili vilivyomsababishia majeraha akiwa anashikiliwa na askari wa jeshi la polisi mkoani Morogoro “,amesema.
Kuhusu chunguzi zilizohusu matumizi mabaya ya madaraka THBUB Jaji Mstaafu Mwaimu amesema ilifanya uchunguzi dhidi ya Mhe. Peuline Gekul kuhusu tukio la kuwaingiza chupa sehemu ya aja kubwa Bw. Hashim Ally na Bw. Michael Isaria na kubaini kuwa suala hilo halikufanyika.
“Hata hivyo THBUB ilibaini kuwa walalamikaji walizuiliwa kwa muda mrefu wakati wakihojiwa na mlalamikaji kuhusu tuhuma za kutaka kumwekea sumu Bi. Gekul pamoja na kupekelewa madawa ya kishirikina katika hotel yake na hivyo kusababisha walalamikajj kukosa haki yao ya kuwa huru”,amesema.
Aidha ameongeza kuwa uchunguzi mwingine ni kuhusiana malalamiko dhidi ya mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda kuhusu kutoa amri ya kukamatwa na kuwekwa ndani ya mahabusu ya polisi mkazi mmoja wa Arusha na kubaini kuwa amri iliyotolewa haikuwa halali na haikuzingatia aina ya makosa.
Amesema Tume itaendelea kufanya uchunguzi katika matukio yanayojitokeza na yenye viashiria vya uvunjifu wa amani nchini ili kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa mara moja katika jamii.