TIRA YALIPA MIL 500 ZA BIMA YA MAZAO YA WAKULIMA

Na Lucas Raphael ,Tabora

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewalipa wakulima wa zao la tumbaku kutoka Mikoa ya Tabora, Kigoma, Mbeya na Shinyanga sh mil 500 kama fidia ya mazao yao yaliyoharibiwa na majanga ya mvua na ukame.

Hayo yamebainishwa jana na Kamishna Mkuu wa TIRA Dkt. Baghayo Saqware alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) katika Viwanja vya Nane Nane Ipuli Mkoani Tabora.

Alieleza kuwa katika msimu 2 ya kilimo cha zao hilo 2021/2022 na 2022/2023 wakulima wa Mikoa hiyo wamenufaika na huduma za bima ya kilimo zinazotolewa na Taasisi ya TAIC chini ya usimamizi wa TIRA.

Dkt Saqware alisema kuwa serikali imeanzisha Mamlaka hiyo ili kuonesha jinsi inavyowajali wakulima na dhamira yake ya dhati ya kuwainua kiuchumi kupitia shughuli zao za kilimo na haitaki jasho lao lipotee.

Aliongeza kuwa serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuhakikisha bima inapatikana kwa bei nafuu kwa wakulima wakubwa na wadogo ambao ndio wengi .

Aidha alibainisha kuwa TIRA kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta na wadau wengine wanaendelea na mchakato wa kuanzishwa Skimu ya Bima ya Kilimo Tanzania ili kupanua wigo wa utoaji huduma hizo kwa wakulima.

Saqware alifafanua lengo la kuanzishwa mpango huo kuwa ni kulinda maslahi ya wakulima wote nchini dhidi ya athari za majanga mbalimbali yanayoweza kuikumba sekta hiyo.

Alitaja baadhi ya majanga hayo kuwa ni mafuriko, ukame, magonjwa na wadudu waharibifu na kusisitiza dhamira yao ya kuongeza upatikanaji mikopo kwa wakulima wadogo na huduma za bima ya kilimo kwa bei nafuu sana.

 Meneja wa TAIC Mkoani Tabora Prospar Peter alisema kuwa TAIC inashirikiana na kampuni mbalimbali zinazotoa huduma za bima ya kilimo kwa wakulima hapa nchini.

 Mkurungezi Mkuu wa Kampuni Tanzu ya Bima ya CRDB Wilson Mnzava alisema kuwa wao wanatoa bima za mazao, mifugo, uvuvi na misitu kwa wakulima wadogo na wakubwa.Kamishna wa Bima Tanzania Dkt. Baghayo Saqware, akiwa na watumishi mbalimbali wa serikali na wadau wa TIRA katika Siku ya Ushirika Duniani  iliyofanyika katika uwanja wa Fautuma mwasa mkoani Tabora

 

Previous Post Next Post