TPDC YAUNGA MKONO MPANGO WA NISHATI SAFI NCHINI

 



"Ujenzi wa Kituo mama cha kushindilia gesi asilia kwenye magari (CNG) ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha Watanzania wote wanatumia nishati safi kwenye magari, kupikia na vyombo vingine vya moto".

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. James Mataragio wakati alipotembelea eneo la ujenzi wa Mradi wa Kituo Mama cha kujaza gesi asilia kwenye magari (CNG) leo tarehe 18.07.2024 eneo la Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.

"Serikali ina mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo tunategemea kwamba ndani ya miaka 10 kuanzia 2024-2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, Serikali iko mstari wa mbele kuhakikisha usambazaji wa nishati safi unawafikia Wananchi katika maeneo mbalimbali", amesema Mataragio.

Dkt. Mataragio amesema Mradi huu utachochea usambazaji na upatikanaji wa nishati safi kwenye maeneo yote ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya gesi, mradi wa CNG utasafirishwa kwa kutumia magari kwenda mikoa ya Dodoma na Morogoro pamoja na mikoa mingine ambayo haijafikiwa na miundombinu ya gesi asilia.

Naye, Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini -TPDC Mhandisi Emmanuel Gilbert amesema ujenzi wa kituo hicho utawezesha gesi kupatikana maeneo ambayo gesi haijafika kabisa. "Mtu anaweza asione bomba Morogoro lakini baada ya kituo hiki kukamilika gesi itakuwa na uwezo wa kufika Morogoro na Mikoa mingine Tanzania".

Aidha,Gilbert amewaomba wenye vituo vya mafuta katika maeneo mbalimbali kuongeza mfumo wa kujaza gesi asilia kwenye vituo vyao kwa kuingia mkataba na TPDC wa kuchukua gesi asilia kwenye Kituo Mama cha CNG na kuuza kwenye vituo vyao.

Kituo Mama cha CNG kitakuwa na uwezo wa kujaza gesi asilia kwenye magari maalumu ya kusambaza na kusafirisha gesi, kujaza gesi asilia kwenye magari yanayotumia gesi, karakana ya kuweka mifumo ya gesi kwenye magari.
Previous Post Next Post