Ticker

6/recent/ticker-posts

WATENDAJI WATAKIWA KUWA NA USHIRIKIANA JAJI JACOBS MWAMBEGEKE

Na Lucas Raphael, Tabora  

 

Watendaji wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Tabora na Katavi wametakiwa

kuwa na ushirikiano kati yao, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi.

 

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegeke wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo katika ukumbi wa mikutano wa Isike Mwanakiyungi  Mkoani Tabora.

 

Alisema kwamba matokeo bora ya zoezi hili yanategemea kuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya watendaji  wa uboreshaji, Serikali, Vyama vya Siasa na wadau wengine wa uchaguzi.

 

Jaji Mwembegele aliwataka watendaji hao kuwa na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao na ikiwa wanahitaji ufafanuzi au maelekezo yeyote, wasisite  kuwasiliana na Tume.

 

Aidha, alisema wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa Vyama vya Siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura jambo ambalo litasaidia kuleta uwazi katika zoezi hilo.

 

“Mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima. Mawakala hao hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni,”alisema Jaji Mwambegele.

 

Katika hatua nyingine alisema Tume ilitoa vibali kwa Asasi za kiraia 157 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na waangalizi wa zoezi la uboreshaji 33 watakao tazama zoezi la  uboreshaji.

 

Jaji huyo  alisema kuwa Tume inasisitiza kwa Maafisa Waandikishaji kuwa, wanapofika katika maeneo yao, wapewe ushirikiano kwa kuwa ni wadau muhimu.

 

Hata hivyo Tume imetangaza uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika Julai 20, 2024 mkoani Kigoma ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na kauli mbiu ya uboreshaji ni “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi Wa Uchaguzi Bora”.

 

Mafunzo kama hayo pia yamefanyika Mkoa wa Katavi na na kufunguliwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari na yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 20 hadi 26, 2024. 

 

Post a Comment

0 Comments