WAZIRI MAVUNDE AAGIZA LESENI ZA UTAFITI 45 MKOANI RUKWA KUREJESHWA SERIKALINI

 

-Ni Leseni ambazo hazifanyiwi kazi na kuzuia maelfu ya wachimbaji kuchimba


-Eneo lililorejeshwa la ekari 812,383 ni kubwa zaidi ya Wilaya ya Sumbawanga

-Wachimbaji wadogo na wawekezaji waliotayari kupewa kipaumbele kwenye ugawaji

-Serikali kuchochea shughuli za uchimbaji madini mkoani Rukwa

Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema serikali imefuta na kurejesha serikali Leseni za Utafiti 45 kati ya 102 zilizopo mkoani Rukwa kwa kushindwa kufanyiwa kazi na kukidhi masharti yaliyowekwa.

Waziri Mavunde ameyasema hayo jana Wilayani Sumbawanga,wakati akijibu hoja za uongozi wa wachimbaji mkoani Rukwa ya ombi la kupatiwa maeneo ya uchimbaji katika kikao kilichofanyika kati ya Waziri wa Madini na wadau wa sekta ya madini mkoani Rukwa.

“Mh Rais Dkt. Samia S. Hassan ametupa maelekezo bayana ya kuhakikisha Leseni zinatolewa zinafanya kazi na watu wasihodhi maeneo makubwa bila kuyafanyia kazi ili kuchochea shughuli za uchimbaji na ukuaji wa sekta ya madini.

Hapa Mkoani Rukwa tumerejesha Leseni 45 Serikalini ili kutoa fursa kwa Serikali kuyapanga vyema maeneo hayo kwa kutenga Leseni kwa ajili ya wachimbaji wadogo na wawekezaji wakubwa walio tayari kuwekeza kwenye sekta ya madini.

Leseni hizi 45 tu zilikuwa zimeshikilia eneo kubwa la ekari 812,383 ambalo ni kunwa kuliko eneo la Wilaya nzima ya Sumbawanga ambayo ina eneo la ukubwa wa ekari 667,641.

Uchimbaji hapa mkoani Rukwa upo chini,hivyo ni jukumu la Ofisi ya Afisa Madini Mkoa kuhakikisha mnachochea shughuli za uchimbaji hapa mkoani Rukwa”Alisema Mavunde

Naye Afisa Madini wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Joseph Kumburu amemuhakikishia Waziri Mavunde kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo hasa la kuchochea shughuli za uchimbaji wa madini mkoani hapa kwa kuwa Rukwa imejaaliwa madini mengi ya aina tofauti tofauti na hivyo ina fursa kubwa ya kufanya vizuri zaidi.

Akiwasilisha taarifa ya wachimbaji,Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Mkoani Rukwa(RUREMA) Ndg.Masie D.Mwambegele ameiomba serikali kuwapatia maeneo wachimbaji wadogo katika maeneo ambayo hayafanyiwi kazi na kuomba serikali iongeze nguvu kwenye eneo la utafiti ili wachimbaji wasichimbe kwa kubahatisha kama ilivyo sasa.







Previous Post Next Post