WAZIRI MKUU: MA-RC, MA-DC HAKIKISHENI MIRADI YA MAENDELEO INAKAMILIKA





Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza kwa njia ya mtandao (Video Conference) na Viongozi wa Chama Mikoa, Kamati za Usalama Mikoa na Wakuu wa Wilaya Tanzania Bara, kwenye ukumbi wa Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam Julai 22.2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…………….

*Asisitiza ianze kutoa huduma kwa wananchi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasimamie miradi yote ya maendeleo kwenye mikoa na wilaya zao na kuhakikisha inakamilishwa ili ianze kutoa huduma kwa wananchi.

“Kwenye eneo la usimamizi wa miradi, Wakuu wa Mikoa hakikisheni mnazo taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo; hii ni fursa yenu ya kujua benki tuliyonayo ya utekelezaji wa miradi yote ya tangu mwaka 2021. Angalieni ni miradi gani imepata fedha, na mjiridhishe kama imekamilika au la, na kama bado haijakamilika, fuatilieni ni kwa nini haijakamilika.”

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Julai 14, 2024) wakati akizungumza na Kamati za Usalama za Mikoa na Wilaya Pamoja na viongozi wa CCM wa Mikoa kwenye kikao kazi alichokiendesha kwa njia ya mitandao (video conference) kutokea ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Magogoni, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema miradi inayojengwa kwa fedha za Serikali kwenye Halmashauri na Manispaa ni mingi hivyo amesisitiza ikamilishwe kwa asilimia 90 ifikapo Desemba, 2024 ili ianze kutumika mapema. “Matumizi ya miradi hii, ndiyo faraja kwa wananchi na ndiyo matamanio yao,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahimiza viongozi hao wafuatilie uzalishaji wa chakula ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na ziada ya kutosha. “Tanzania tumezalisha chakula kingi na tuna ziada; Wakuu wa Mikoa na Wilaya jukumu lenu kusimamia kilimo na uzalishaji uwe umefikia malengo na wenye ziada. Pia fanyeni sensa ya kujua mazao ya kwenye maghala, uhifadhi wake ni mzuri, na je kinatosha? Tuwe na takwimu za kutosha juu ya chakula tulichonacho kwenye hifahi yetu,” amesisitiza.

Wakati huohuo, Wazri Mkuu Majaliwa amesisitiza kwamba makusanyo yote ya fedha kwenye Halmashauri na Manispaa ni lazima yaingizwe benki ndipo yapangiwe matumizi. “Hata kama zi fedha za msaada kutoka kwenye taasisi au asasi zisiso za Kiserikali, ni lazima DC ajue ili atoe taarifa kwa RC. Ma-RC wasimamie mtiririko wa fedha kwenye Halmashauri.”

“Suala la usimamizi wa mapato ya Serikali iwe ajenda ya kudumu. Tusipofanya hivyo, tutashindwa kutekeleza mipango yetu. Mmemsikia Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akisisitiza kuhusu ukusanyaji wa mapato, mapato ambayo baadaye yanaletwa kwenye maeneo yenu ili kutekeleza miradi.”

Maeneo mengine aliyoyawekea msisitizo kwenye kikao hicho ni pamoja na utatuzi wa kero za wananchi, udhibiti na uhifadhi wa mazingira, nishati safi ya kupikia, ulinzi na usalama, kilimo cha umwagiliaji, magonjwa yasiyoambukiza, maandalizi ya AFCON 2027 na ushirikiano baina ya viongozi wa Serikali na wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kikaokazi hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi (OWM-SBU), Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Mohammed Mchengerwa
Previous Post Next Post