WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAPONGEZWA KWA LADHA YA UTALII WA UTAMADUNI MAONESHO YA SABASABA

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini (Mb) ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuweka vionjo vya utalii wa utamaduni hasa wa kabila la Wazanaki kama nyumba na vitu vya asili vya kabila hilo lenye asili ya Butiama, Mkoani Mara.Ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Sabasaba mara baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Maonesho hayo akiwa na mgeni wake Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji ambaye alikuwa mgeni rasmi.“Nimevutiwa sana kukuta kabila la Wazanaki na mimi nikashiriki katika kusaga chakula lakini pia nikaona nyumba na kitanda cha miti kama kilivyokuwa kinatumika na wazee wetu wa zamani “ amesisitiza Mhe. Sagini.Amesema kupitia maonesho hayo Watanzania  wataweza kuona vitu ambavyo jamii za zamani zilikuwa zikiishi na kuwahimiza Watanzania kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.Aidha, ameishauri Wizara hiyo kuangalia namna ya kuweka taarifa za utalii wa utamaduni kidijitali kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.Naye, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Mhandisi Ezra Chiwelesa amewahamasisha Watanzania kutenga muda kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii ili waweze kujionea mambo mbalimbali ikiwemo  viumbe hai kama nyoka wa aina mbalimbali, fisi,  chui na wengine.Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.  Angellah Kairuki (Mb) ameongozana na Mhe. Sagini, Mhe. Chiwelesa pamoja na viongozi wengine wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii.

 

Previous Post Next Post