BARAZA LA MADIWANI LA HALMASHAURI YA MANISPAA YA SHINYANGA LAPONGEZA MKURUGENZI KWA MAFANIKIO YA UKUSANYAJI MAPATO

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mheshimiwa Elias Ramadhan Masumbuko akimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga leo Alhamisi Agosti 29,2024.

Na Mapuli Kitina Misalaba

 Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga limepongeza kwa dhati juhudi za Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mwalimu Alexius Kagunze, kwa kuleta mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2024.

Pongezi hizi zilitolewa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mheshimiwa Elias Ramadhan Masumbuko, katika mkutano maalumu wa Baraza hilo uliofanyika kwa lengo la kujadili taarifa za hesabu za mwisho za Halmashauri hiyo.

Meya Masumbuko ameainisha mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Mkurugenzi Kagunze, ambapo ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka Shilingi bilioni mbili hadi bilioni tano.

"Mimi ninayo kumbukumbu nzuri sana ya jinsi tulivyoanza. Wakati tumeingia hapa, tulikuwa tunakusanya bilioni mbili, wakati makisio yalikuwa bilioni tatu, leo hii, tunakusanya bilioni tano hatujabadilisha vyanzo, hatujaongeza kodi, wala hatujamsumbua mwananchi kulipa zaidi, mafanikio haya yanatokana na usimamizi bora wa timu ya Mkurugenzi," amesema Meya Mhe. Masumbuko.

Aidha, Meya huyo ametoa shukrani kwa Mbunge wa jimbo la Shinyanga Mjini, Mheshimiwa Paschal Patrobas Katambi, kwa mchango wake katika kufanikisha malengo ya kimahesabu ya Halmashauri hiyo.

"Licha ya majukumu yake mawili, Mheshimiwa Katambi amekuwa na mchango mkubwa sana katika kufanikisha ukusanyaji huu wa mapato."amesema Masumbuko

Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ilikisia kukusanya jumla ya Shilingi bilioni 5.6 kutoka vyanzo vya ndani hadi kufikia Juni 30, 2024, Halmashauri ilikuwa imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 5.535, sawa na asilimia 98.85 ya makisio.

Taarifa hiyo ya mwisho ya hesabu za Halmashauri ilionyesha pia ongezeko la mali za kudumu kutoka Shilingi bilioni 173.3 hadi bilioni 176.1. Mweka Hazina wa Halmashauri, CPA Mulokozi Kisenyi, amesema ongezeko hili limetokana na uwekezaji kwenye majengo, miundombinu ya shule na afya, pamoja na ununuzi wa samani na vifaa vya ofisi.

"Pamoja na changamoto zilizopo, tumefanikiwa kuongeza mali za kudumu kutoka Shilingi bilioni 173.3 hadi bilioni 176.1, ongezeko linalotokana na kuongezeka kwa majengo na miundombinu muhimu," amesema Kisenyi.

Kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2024, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga iliidhinishiwa kupokea kiasi cha Shilingi bilioni 9.567 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo hadi kufikia tarehe hiyo, Halmashauri ilifanikiwa kupokea kiasi cha Shilingi bilioni 10.949, sawa na asilimia 114.45.

Fedha hizo zimetumika katika utekelezaji wa miradi kadhaa muhimu, ikiwemo Mfuko wa TASAF, Mfuko wa Jimbo, Mfuko wa Afya wa Pamoja (HSBF), pamoja na miradi ya elimu na afya, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya shule na zahanati.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mwalimu Alexius Kagunze, amesisitiza kuwa wataendelea kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali ili kuendeleza maendeleo kupitia mapato ya ndani.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mheshimiwa Anord Makombe, ameitaka Halmashauri hiyo kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato, akisisitiza umuhimu wa kuimarisha misingi ya uwajibikaji na uadilifu katika ukusanyaji huo.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mheshimiwa Elias Ramadhan Masumbuko akizungumza kwenye mkutano maalumu wa Baraza leo Alhamisi Agosti 29,2024.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Mwalimu Alexius Kagunze akizungumza kwenye mkutano maalumu wa Baraza leo Alhamisi Agosti 29,2024.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mheshimiwa Anord Makombe, akizungumza kwenye mkutano maalumu wa Baraza leo Alhamisi Agosti 29,2024.


 

Previous Post Next Post