Na Swedi Mbaruku, Misalaba Media
Mchezo wa nusu fainali ya kwanza wa Dkt. Samia Katambi
Cup 2024 umemalizika leo nakuacha gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka,
baada ya timu ya Ngokolo FC kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Kolandoto
FC katika uwanja wa Shycom, Manispaa ya Shinyanga.
Mchezo huo uliochezwa majira ya saa kumi jioni,
ulishuhudia ushindani mkali na nidhamu ya hali ya juu kutoka kwa timu zote
mbili, kutoka mwanzo hadi mwisho, timu zilionesha kiwango bora cha soka, zikiwania
tiketi ya kufuzu hatua ya fainali ya michuano
hii katika Manispaa ya Shinyanga.
Dakika za awali za mchezo huo zilikuwa na msisimko mkubwa,
huku wachezaji wa timu zote mbili wakionyesha ujuzi wao wa kusakata kabumbu.
Hata hivyo, ilikuwa ni nafasi moja ya dhahabu
iliyotumiwa vema na Bakari Said, mchezaji wa Ngokolo FC, ambaye aliipatia timu
yake goli la pekee lililowapa ushindi.
Bakari Said, ambaye amekosa mechi kadhaa za awali,
aliibuka shujaa wa mchezo huo baada ya kufunga goli hilo muhimu.
Akiongea baada ya mchezo, Bakari amesema kwamba
mbinu za kocha na mahitaji ya mchezo husika yalikuwa na nafasi kubwa katika
ushindi huo. "Unajua huwezi kuingia vitani na silaha zote, kwa hiyo
mwalimu na menejimenti wameliangalia hilo, ndio maana huko nyuma
sikuonekana," amesema Bakari kwa kujiamini.
Kwa upande wa Kolandoto FC, licha ya juhudi zao
kubwa za kurejea mchezoni, hawakuweza kubadili matokeo ambapo nahodha wao,
Jummanne Tunze, alikiri kuwa goli la mapema la Ngokolo FC lilikuwa na athari
kubwa kwenye mchezo wao, ingawa timu yake ilijitahidi kucheza kwa nidhamu na
umakini mkubwa.
"Goli
walilolipata Ngokolo katika dakika za awali ndio lililotupa ugumu, licha ya kucheza
vizuri na kwa nidhamu," amesema Tunze kwa masikitiko.
Mashabiki walioshuhudia mchezo huo walikubaliana
kuwa ulikuwa ni moja ya mechi bora zaidi katika michuano ya mwaka huu, huku
wakisubiri kwa hamu nusu fainali ya pili.
Mchezo wa nusu fainali ya pili ya Dkt. Samia Katambi
Cup unatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi tarehe 17 Agosti 2024 katika uwanja
wa Shycom, ambapo Masekelo FC watapambana na KASHUWASA.
Timu hizo mbili zitakutana kuwania nafasi ya kucheza
fainali dhidi ya Ngokolo FC, mchezo unaotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa
kutokana na historia na ushindani wa timu zinazoshiriki.