Na Mwandishi Wetu

MWAKA 1994 hauwezi kufutika katika historia ya dunia baada ya watu zaidi ya 800,000 kupoteza maisha kwa mauaji ya wenyewe kwa wenyewe nchini Rwanda. Wengine zaidi ya 2,000,000 walikimbia nchi na kwenda maeneo mbalimbali duniani kuomba hifadhi.

Sababu ya yote hayo ni kauli. Wahutu na Watusti walianza kutoleana kauli za vitisho na kila mmoja kujiona bora zaidi ya mwenzake. Baadaye walichinjana na kuuana watu wa famailia moja.

Nchini Kenya mnamo mwaka 2007 vurugu baada ya uchaguzi mkuu uliomuweka madarakani hayati Mwai Kibaki, zaidi ya watau 1,000 walipoteza maisha. Inadaiwa zaidi ya wanawake 1,200 walibakwa, idadi ya waliojeruhiwa haijulikani na zaidi ya watu 300,000 walikosa mahali pa kuishi.

Haya yote yalianzishwa na kitu kimoja tu, kauli. Kauli za wanasiasa ni upanga wenye makali kuliko risasi.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kinailalamikia Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa haitimizi wajibu wake katika haki za binadamu. Lakini wanasahau kitu kimoja kuwa wajibu unatimizwa kwa pande zote mbili.

Mwishoni mwa wiki Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, Benson Kigaila alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, juu ya kukamatwa viongozi wa chama chake na baadhi ya wananchama mkoani Mbeya wakati wakijiandaa na mkutano wa siku ya vijana waliopanga kuufanya Uwanja wa Ruanda Nzomve mkoani Mbeya, Agosti 12, 2024.

Awali, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo Jeshi la Polisi Tanzania, Awadh Juma Hajji alitoa tamko la kuzuia mkutano huo akieleza kuwa kulikuwa na harufu ya uvunjifu wa amani. Akaagiza pia mabasi zaidi ya 200 yaliyokuwa njiani kutoka mikoa mbalimbali kwenda Mbeya nayo yazuiwe.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa BAVICHA, Moza Ally alitoa tamko vijana wote waliokuwa njiani kwenda Mbeya kwa mabasi wazime magari wafunge barabara ili kusitisha shughuli zote siku ya Jumamosi na Jumapili yaani Agosti 10 na 11, 2024.

Mambo haya yanaendana kinyume kabisa na kauli za pamoja zilizotolewa Januari 2023, Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam wakati Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipowaita viongozi wa vyama vyote vya siasa vyenye usajili nchini kuzungumza nao, ambapo hadi viongozi wa Chadema walihudhuria.

Siku hiyo Rais Samia alikutana na vyama vya siasa nchini ambapo mbali ya mambo mengine alimaliza kifungo cha takriban miaka sita kilichowekwa na mtangulizi wake Hayati Dk. John Magufuli juu ya mikutano ya vyama vya siasa.

Aliruhusu siasa za majukwaani zifanyike, lakini alitoa angalizo kuwa uhuru una mipaka yake na haki inaendana na wajibu. Hivyo, siasa za majukwaani zifanyike kwa ustaarabu na kutumia lugha za staha. Si matusi wala kudhalilishana.

“Hii ni haki kwa sheria zetu, ni haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara, uwepo wangu leo mbele yenu ni kuja kutangaza, lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoka,” alisema Rais Samia na kusisitiza:

“Lakini ndugu zangu tuna wajibu, wajibu wetu serikali ni kulinda mikutano ya vyama vya siasa, wajibu wenu vyama vya siasa ni kufuata sheria na kanuni zinavyosema, twendeni tukafanye siasa za kistaarabu, tukafanye siasa za kupevuka, tukafanyeni siasa za kujenga si za kubomoa, sio kurudi nyuma hapa tulipofika, sisi ndani ya CCM tunaamini katika kukosolewa na kujikosoa.”

Kwa mtu muungwana na mwenye nia njema na nchi yake, haya maneno yangetosha kuwa mkataba wa amani kwa wakati wote nchini.

Lakini zuio la Jeshi la Polisi linatokana na kauli za viongozi wa BAVICHA, ikiwemo hizi:

“Kama kijana yeyote unayeipenda nchi yako ya Tanzania umeshalia miaka yako yote, siku hiyo ya Agosti 12, 2024 tunakwenda kuweka hatma ya taifa letu la Tanzania mkoani Mbeya, kwa hiyo kijana yeyote uliyepo popote Tanzania njoo Uwanja wa Ruanda Mzomve, Mbeya.

“Tupo Serious na jambo hili, kwa hiyo vijana wote wa CHADEMA kama ambavyo vijana wa Kenya wamejitambua siku ya Tarehe 12/08/2024 tunakwenda kuacha uteja kwa serikali, vijana wa Kitanzania na kuweka maazimio makubwa ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2025.”

Kauli kama hizi si za kuzipuuza, Tanzania ni moja ya mataifa yanayosifiwa kwa utulivu. Yanayosifiwa kwa amani na kila lililo jema. Haiwezekani watu wachache wenye nia ovu wavuruge misingi imara ya taifa hili iliyojengwa na watangulizi wetu.

Hakuna mahali vyama vya siasa vimezuiwa kufanya siasa. Tumeshuhudia viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini wakizungumza kwenye majukwaa kwa nyakati tofauti, tangu kufunguliwa mikutano ya hadhara.

Iweje Jeshi la Polisi libadili kauli yake? Unadhani Jeshi la Polisi linaweza kukiuka amri ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan?

Ni wazi lipo jambo haliko sawa kiusalama. Hatua sahihi lazima zichukuliwe kwa wakati kabla mambo hayajaharibika.