Na Mapuli Kitina Misalaba
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imefanya kongamano
la vijana katika uwanja wa Stendi ya Songambele, kata ya Salawe, ambapo elimu
ya uzalendo wa Mwenge wa Uhuru imewasilishwa na kujadiliwa kwa kina.
Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi wa
serikali, taasisi binafsi, wadau kutoka mashirika mbalimbali, pamoja na vijana,
wanawake, wazee, na wananchi kwa ujumla.
Katika kongamano hilo, elimu ambayoimetolewa imeambatana
na mijadala mbalimbali, ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa, ukatili wa
kijinsia, uhifadhi mazingira, masuala ya kiuchumi, na fursa mbalimbali
zinazowakabili wananchi ambapo washiriki wamesisitizwa umuhimu wa kuendelea
kuwa wazalendo wa kweli ili kuendeleza amani ya taifa la Tanzania.
Afisa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga
Oscar Lupama, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika
daftari la wapiga kura ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa
serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu 2024.
"Kila
raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 na kuendelea ana haki na wajibu wa
kushiriki katika uchaguzi huu kwa amani na utulivu kama ilivyokusudiwa."
Amesema,
Aidha, Lupama ametumia nafasi hiyo kutaja sifa za
mpiga kura na mgombea, akieleza kuwa lazima awe Mtanzania mwenye umri wa miaka
21 na kuendelea, na awe na ujuzi wa kusoma na kuandika angalau lugha mbili,
Kiswahili na Kiingereza ambapo amewasisitiza wananchi kuzingatia sifa hizo ili
waweze kuchagua viongozi bora.
Mwakilishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga Bi. Alicia John, amewataka wananchi kujiepusha na
vitendo vya rushwa hasa kipindi cha uchaguzi, akisisitiza kuwa ni jukumu la
kila mmoja kuzuia rushwa ili kuepusha migogoro na athari mbalimbali za
maendeleo.
"Wapiga kura wanapaswa kutumia haki yao
ipasavyo kwa kuchagua viongozi bora na waadilifu ili kutatua kero
zinazowakabili." Amesema,
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Godfrey
Eliakimu Mnzava, ametoa pongezi kwa kufanyika kwa kongamano hilo na amesisitiza
umuhimu wa wananchi kuendelea kuwa wazalendo ili kuendeleza amani na umoja
ndani ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga, Dkt. Kalekwa Kasanga, Mwenge wa Uhuru umekimbizwa kwa kilomita 160
katika Halmashauri hiyo, ukimulika miradi 14 ya maendeleo yenye thamani ya
shilingi bilioni 1.7.
Miradi yote ambayo imepitiwa na Mwenge wa Uhuru 2024
katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, imepita bila kupingwa jambo
linaloashiria mafanikio makubwa katika jitihada za maendeleo wilayani humo.
Kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru 2024
inasema"Tunza mazingira na Shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa
ujenzi wa taifa endelevu".