KUNDO AKATAA WANAOUNGANISHA MAJI KULAZIMISHWA KUTUMIA VIFAA VYA MAMLAKA


NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew amekemea ucheleweshaji wa kufungia wateja huduma ya maji na wakati huo huo kuzuia utaratibu wa Mamlaka hizo hapa nchini kuwalazimisha wale wanaounganishiwa huduma hizo kutumia vifaa vyote toka idara hiyo.

Mhandisi Kundo alilazimika kutoa kauli hiyo jana Jijini Mwanza kufuatia kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wakaazi wa Kata ya Buhongwa juu ya ukosefu wa maji kwenye eneo hilo na kuwasababishia adha mbalimbali za kimaisha.

Alisema hakuna haja kwa Mamlaka za maji kuwalazimisha kutumia vifaa vyote vya idara ya maji badala yake mteja aweze kuwa na fursa ya kulinganisha unafuu wa bei ya bidhaa hizo katika pande mbili tofauti.

Kuhusiana na adha ya ukosefu wa maji Naibu Waziri Mhandisi Kundo alisema serikali inatarajia kuanza ujenzi wa mradi mkubwa wa maji kwenda wilayani Misungwi wenye thamani ya bilioni 49.9 ambao utakamilika baada ya miezi 18 na hivyo kuondoa tatizo hilo la maji.

Aidha Mhandisi Kundo alisema kwa sasa mpango wa muda mfupi ni ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kutunza lita milioni 2 katika eneo la Sawa ambapo litaanza kutoa huduma baada ya miezi miwili.

Diwani wa Kata ya Buhongwa Joseph Kabati alilalamikia kuwepo kwa baadhi ya watu wanaoendesha biashara ya kuuza maji kupata huduma hiyo bila kuathirika na mgawo huku wengine wakikoswa maji.

Alisema kuna haja ya kuwepo uangalizi kufahamu ni kwa nini wasiouza maji wengi wao wanaathiriwa na mgawo wa maji kwa muda mrefu tofauti na wenye kufanya biashara hiyo.
Previous Post Next Post