MAKONDA AIBUKIA UWANJA WA NDEGE ARUSHA...AAGIZA JENGO JIPYA LIANZE KUTUMIKA SEPTEMBA 1


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Christian Makonda leo Ijumaa Agosti 16, 2024 ameagiza kukamilika haraka kwa ujenzi wa jengo la abiria kwenye uwanja wa ndege wa Arusha (Kisongo), ili kuwezesha jengo hilo kuanza kufanya kazi Septemba Mosi mwaka huu.

Mhe. Makonda ametoa maagizo hayo wakati alipofika kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la abiria ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia kwa wakati mmoja abiria takribani 1000 tofauti na jengo la awali lililokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 150 pekee.

“Shauku yetu sisi wananchi wa Mkoa wa Arusha ni kuwa uwanja wetu huu uweze kufanya kazi kwa saa 24 na wale wenye ndege zao binafsi waweze kutumia uwanja wetu ili kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye lengo lake ni kuufungua mji wa Arusha na kuongeza hamasa ya watalii kuja nchini mwetu.” amesema Mhe. Makonda.

Katika hatua nyingine, Makonda pia ameagiza kutumika kwa teknolojia katika utoaji wa huduma kwa abiria wanaotumia uwanja huo pamoja na kuweka miundombinu ya kutangaza utalii wa Arusha, ili kuvutia zaidi watalii wanaofika Mkoani hapa kuweza kutembelea vivutio vinavyopatikana na mkoani Arusha na mikoa ya pembezoni.
Previous Post Next Post