MAONO YA RAIS SAMIA YAZIDI KULETA WATALII NCHINI TANZANIA


Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutengeneza filamu ya Tanzania The Royal Tour yameendelea kuongeza idadi ya wageni nchini ambapo Agosti 27,2024 Tanzania imepokea taasisi na makampuni yanayojishugulisha na masuala ya utalii kutoka nchini Brazil.

Ameyasema hayo katika hafla ya chakula cha usiku ya wageni hao kutoka nchini Brazil, usiku wa Agosti 27,2024 katika hoteli ya Forest Hill jijini Arusha.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa maono yake makubwa ya kuja na filamu maalum ya Tanzania the Royal Tour ambayo inaendelea kuitangaza Tanzania katika soko la utalii la dunia na chini ya uongozi wake nchi ina amani na utulivu na hivi sasa tunapata wageni wengi sana watalii na ninafurahi kusikia hiki ni kipindi cha watalii wengi” amesisitiza Mhe. Chana.

Ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia watanzania kwamba Sekta ya utalii inaendelea vizuri  na kwamba wageni hao wamekuja kujifunza masuala mbalimbali  Tanzania ikiwa ni pamoja na kutembelea vivutio vya utalii na pia kushirikiana na Wakala wa Usafirishaji Watalii nchini.

Amefafanua kuwa Tanzania imeendelea kuwa na mahusiano imara ya kidiplomasia kati yake na Brazil hivyo itakuwa rahisi kuleta  na kurahisisha upatikanaji wa visa baina ya nchi hizo mbili na kuwakaribisha wageni hao kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, amewakaribisha wageni hao kujionea vivutio vingi vilivyopo nchini Tanzania na kusisitiza kuwa matarajio yake baada ya Safari hiyo ni kuongezeka kwa wasafiri zaidi kutoka nchini Brazil.

Naye, Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Mhe. Profesa Adelardus Kilangi, amesema ujio wa wageni hao ni moja ya mafanikio na hatua muhimu katika kukuza uhusiano kati ya Brazil na Tanzania hasa katika Sekta ya Utalii.

Amesema  madhumuni ya msingi ya  wageni hao ni kutembelea na kuona maeneo ya vivutio vya utalii na kuwasihi kutumia fursa hiyo kuchunguza maeneo mbalimbali ya uwekezaji katika sekta ya utalii.

Kwa upande wake Mratibu wa mawakala hao, Bi. Luciana Teixeiana amefurahishwa na ujio wao nchini Tanzania na kwamba wanahitaji  kujifunza ni kwa namna gani Tanzania inakuza biashara  bila kuharibu mazingira asilia na wanyama, kuijua nchi ya Tanzania zaidi na kwenda kuitangaza.



















Previous Post Next Post