Mashindano ya timu za mpira wa miguu ya The Angeline Ilemela Jimbo Cup 2024 kwa msimu wa nane yamezinduliwa rasmi Leo Agosti 17, 2024 katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Katibu tawala wa wilaya ya Ilemela Wakili Bi Mariam Abubakar Msengi amewataka Vijana wa Jimbo hilo kutumia fursa hiyo kuonyesha vipaji vyao ili kupata nafasi ya kusajiliwa na vilabu vikubwa nchini pamoja na kujiingizia kipato
'.. Michezo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi, Na michezo hii inatuunganisha, ni afya na ni ajira hivyo tuutumie vizuri msimu huu .' Alisema
Aidha Wakili Msengi ameipongeza kauli mbiu ya mashindano hayo kwa msimu huu ya 'Uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024, Tunaanzia tulipoishia' huku akiomba wananchi kujitokeza na kujiandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura litakaloanza mapema Agosti 21 wiki ijayo wilayani humo
Kwa upande wake afisa michezo wa manispaa ya Ilemela Ndugu Bahati Sosho Kizito mbali na kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo kwa kuasisi mashindano hayo ameongeza kuwa Ilemela ni kitovu cha kuibua vipaji vya michezo katika mkoa wa Mwanza akitolea mfano mashindano ya shule za msingi na sekondari UMITASHUMTA na UMISETA kwa namna timu za wilaya hiyo zinavyofanya vizuri sanjari na kutoa wachezaji wengi kuunda timu za mkoa na taifa kutokana na umahiri wa wachezaji wake hivyo kuwaomba wachezaji kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za michezo ili kujiongezea uwezo na umahiri
Charles David Karoli ni Katibu wa mbunge Jimbo la Ilemela ambapo amesema kuwa mashindano hayo kwa msimu wa mwaka huu yatahusisha timu 24 zikiwemo timu 19 zinazoundwa na kata zote za Jimbo hilo, timu moja inayoundwa na kisiwa cha Bezi pamoja na timu nyengine 4 mpya ambazo hazikuwepo hapo awali za wasanii, boda boda, machinga na wafanyabiashara wa mnadani huku timu zote zikikabidhiwa vifaa vya michezo kama jezi na mipira kurahisha ushiriki wao katika mashindano