Na Mapuli Kitina Misalaba
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeendelea na mafunzo maalum kwa ajili ya Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mkoa wa Shinyanga.
Mafunzo hayo kwa siku ya leo Agosti 10, 2024 yamewahusisha
Mratibu wa Uandikishaji wa Mkoa, Maafisa waandikishaji, Maafisa Waandikishaji
Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi, na Maafisa TEHAMA wa
Halmashauri za Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza katika Mafunzo hayo Makamu Mwenyekiti wa
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim
Mbarouk amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanaelewa kwa kina
ujazaji wa fomu na matumizi ya mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters
Registration System – VRS), ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha na
kwa usahihi wakati wa zoezi la uboreshaji wa daftari.
"Kuteuliwa
kwenu kunatokana na ujuzi, uwezo, na weledi mlionao katika kutekeleza majukumu
ya kitaifa, ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,"
"Ni
matarajio ya Tume kuwa mafunzo haya yatawajengea umahiri wa kutosha kutekeleza
majukumu yenu na kufanikisha zoezi hili muhimu." amesema
Mhe. Jaji Mbarouk.
Mhe. Jaji Mbarouk pia amesisitiza umuhimu wa
ushirikiano kati ya watendaji wote wa uboreshaji, serikali, vyama vya siasa, na
wadau wengine wa uchaguzi."Matokeo bora ya zoezi hili yanategemea
ushirikiano mkubwa kati ya wadau wote," ameongeza.
Aidha, amebainisha kuwa mawakala wa vyama vya siasa
wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura ili kuhakikisha
uwazi na kuleta amani katika zoezi hilo.
Wakati huo huo, Tume imetoa kibali kwa asasi za
kiraia 157 kutoa elimu ya mpiga kura na asasi 33 kwa ajili ya uangalizi wa
zoezi la uboreshaji, likiongozwa na kauli mbiu "Kujiandikisha kuwa Mpiga
Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora."
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
Mkoani Shinyanga utafanyika sambamba na Mkoa wa Mwanza kuanzia tarehe 21 hadi
27 Agosti, 2024 katika kipindi hicho, vituo vya kuandikisha wapiga kura vitafunguliwa
saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Kwa Mkoa wa Shinyanga, Tume inatarajia kuandikisha
wapiga kura wapya 209,951, ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 ya wapiga kura
995,918 waliopo kwenye daftari la kudumu. Baada ya zoezi hili, Mkoa wa Shinyanga
utakuwa na jumla ya wapiga kura 1,205,869. Vituo 1,339 vitatumika kwa
uandikishaji mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la vituo 122 ikilinganishwa na mwaka
2019/20.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inawataka wananchi wa
Shinyanga na Mwanza kujitokeza kwa wingi kujiandikisha au kurekebisha taarifa
zao ili waweze kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji, na vitongoji
utakaofanyika Novemba 2024, pamoja na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.