Na Mapuli Kitina Misalaba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamsaka mwanaume
anayefahamika kwa jina la Paul, mkazi wa mtaa wa Banduka, kata ya Ndala,
Manispaa ya Shinyanga, kwa tuhuma za kumjeruhi vibaya mtalaka wake, Bi. Ester
Matalanga, kwa kumtoboa Macho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi
Mwandamizi Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa, "Siku ya tarehe 13, Mwezi wa 8, 2024,
majira ya saa kumi na moja na nusu alfajiri, nilipokea simu kutoka kwa
Mwenyekiti wa mtaa wa Banduka akiniarifu kwamba kuna mwanamke ametobolewa macho
na mtu anayesadikika kuwa ni mume wake wa zamani.".
"Kwa
haraka kabisa, jeshi la polisi lilimchukua mwanamke huyo na kumpeleka Hospitali
ya Kolandoto kwa ajili ya matibabu ambapo uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba
tukio hili chanzo chake ni wivu wa mapenzi, na mtuhumiwa ni mlinzi anayefanya
kazi Buhangija., hatuwezi kuvumilia ukatili huu, na tutahakikisha mtuhumiwa
anafikishwa kwenye vyombo vya sheria."amesema Kamanda
Magomi
Mwenyekiti wa mtaa wa Banduka, Bw. Pius Mathias, ameeleza
kwamba alipata taarifa kutoka kwa wakazi wa mtaa wake usiku wa kuamkia jana
ambapo alifanya juhudi za kuwasiliana na polisi.
“Usiku
wa kuamkia jana majira ya saa tisa usiku nilipigiwa simu na wananchi wangu
wanaoishi karibu na bondeni pale mtoni kwamba kuna mwanamke ametobolewa macho
sikuchelewa nikawa nimefika kwenye eneo la tukio ni kweli nikamkuta huyo
mwanamke ambaye alikuwa akijieleza lakini kwa simanzi alikuwa haoni tayari
alikuwa ametobolewa macho yake yote basi baada ya kuona tukio hilo ikabidi
nipige simu polisi”
"Nashukuru Kamanda wa Polisi Mkoa alitoa
ushirikiano wa kutosha, na maafisa wake walifika haraka eneo la tukio na
kumsaidia mwanamke huyo," amesema Mwenyekiti
Pius
Wakazi wa mtaa wa Banduka wameeleza masikitiko yao
juu ya ukatili huo na kuzitaka mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya
mtuhumiwa ili kuhakikisha haki inatendeka.
MISALABA
MEDIA itaendelea kufuatilia tukio hili na kutoa taarifa
zaidi kadri uchunguzi unavyoendelea.