Jeshi la Polisi linamshikilia mwanamume kwa tuhuma za kumuua kwa kumnyonga mkazi wa Mtaa wa Maselele, Kata ya Cheyo B Manispaa ya Tabora, Juliana Mbogo (40) kisha mwili wake kuuficha uvunguni mwa kitanda, chanzo kikidaiwa ni wivu wa mapenzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema hayo leo Jumatano, Agosti 14, 2024 na kuongeza kuwa, mtuhumiwa huyo ambaye jina lake limehifadhiwa alitenda tukio hilo nyumbani kwa mwanamke huyo.
"Ni kweli tunamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kumuua kwa kumnyonga Juliana Mbogo, imeelezwa alimnyonga kwa kamba ya filimbi kisha mwili wake kuuweka chini ya uvungu wa kitanda alichokuwa akilala," amesema.
"Mtuhumiwa alikuwa na uhusiano na Juliana lakini baadaye ukayumba, ndipo akaamua kuja nyumbani kwa Juliana na kumlaghai mtoto wake wa miaka 10 akalale sebuleni, baada ya mtoto kwenda kulala ndipo mtuhumiwa akatekeleza unyama huo.”
Amesema uchunguzi wa kisayansi unaendelea na ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa tuhuma zinazomkabili za mauaji.
Jirani wa marehemu, Elisha Kumbangwa amesema taarifa za kifo cha Juliana alizipata kutoka kwa mtoto wa kwanza wa marehemu mwenye miaka 10.
“Mtoto wa marehemu ametuambia Jumamosi jioni alikuja mtu nyumbani kwao akiwa na mkoba mweusi akajitambulisha kwake kuwa ni mjomba, baada ya hapo mama yake alimkaribisha ndani na ulipofika muda wa kulala, mtoto huyo akaenda kulala akamwacha mama yake na huyo uncle wamekaa sebuleni," amesema Kumbangwa.
Hata hivyo, amesema mtoto huyo aliwaambia ilipofika asubuhi, aliingia chumbani kwa mama yake kuchukua nguo za kuvaa aende kanisani, na alipoingia hakumuona, akaanza kumuita lakini ghafla akatokea mtu akiwa amejifunga kitambaa usoni.
“Mtoto anasema aliogopa akakimbia akatoka nje na kuelekea kwa babu yake anayeishi kilomita kama saba kutoka hapa tunapoishi kutoa taarifa,” amesema Kumbangwa.
Amesema mtoto huyo alipofika na kuwaeleza, wakampuuza huku wakimwambia ana mapepo wakampeleka kuombewa.
Jirani huyo, amesema Jumapili ikapita bila mama huyo kuonekana kwa baba yake, ndipo Jumatatu (Agosti 12) wakafunga safari hadi nyumbani kwa mtoto wao hawakumkuta na walipowauliza majirani nao walikiri kutomuona.
“Na hata walipoingia ndani hawakumkuta, wakaja kwetu kutuuliza tukawaambia hatujamuona, wakaanza kuingiwa na wasiwasi tukashauriana tukatoe taarifa polisi,” amesema Kumbangwa.
Amesema, polisi walifika nyumbani hapo na kuingia chumbani kupekua, wakabaini mwili wa Juliana ukiwa chini ya uvungu wa kitanda.
“Alikuwa amenyongwa na tayari mwili ulikuwa umevimba sana, wakauchukua na kuupeleka Hospitali ya Mkoa wa Kitete,” amesimulia jirani huyo.
John Mbogo ambaye ni baba mdogo wa Juliana, amesema: “Kifo hiki kimeiumiza familia kwa kiasi kikubwa maana tulimtegemea sana, nimefika hospitali nimemuona mwanangu mpaka nimemsahau kwa jinsi alivyovimba, inaumiza sana maana amefariki sio kwa mpango wa Mungu, hata kama wanasema ni wivu wa mapenzi hakukua na haja ya kumuua mtoto wetu tena kwa kumnyonga na kumtupa chini ya kitanda.”
John ameomba sheria ifuate mkondo wake kwa wote waliotekeleza mauaji hayo.
Amesema Juliana ameacha watoto wawili ambao bado walikuwa wanahitaji malezi ya mama yao, “sisi familia inatuuma sana.”
Mwili wa Juliana umezikwa leo Jumatano katika makaburi ya Lwanzari yaliyopo Manispaa ya Tabora.
Mstahiki Meya wa Tabora, Ramadhan Kapera amekemea ukatili dhidi ya wanawake unaoendelea.
Amesema wananchi kwa kushirikiana na vyombo vya dola lazima wavikomeshe.
“Hatuwezi kuendelea kuvumilia ukatili wa aina hii wa kutoana uhai, lazima sheria ifanye kazi,” amesema meya huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Deusdediti Katwale amesema atamsomesha mtoto wa marehemu mwenye miaka 10 mpaka amalize masomo yake.
"Nimeambiwa marehemu ameacha watoto wawili ambao hawana msaada kwa kuwa wamepoteza wazazi, naiomba familia iridhie nikawasomeshe hawa watoto mpaka watakapomaliza elimu zao,” amesema Katwale.
Amesema matukio ya ukatili yameongezeka kwenye jamii, “juzi kuna tukio la mwanamke kuuawa kwa tuhuma za kutembea na waume za watu kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili niwaombe viongozi wa dini wapige magoti kuikemea hali."
CHANZO - MWANANCHI