Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwenge wa Uhuru katika Manispaa ya Shinyanga utawasili Jumapili, Agosti 11, 2024. Mwenge huu utakimbizwa kilometa 74.5 na kutembelea miradi nane yenye thamani ya shilingi bilioni 4.5 ambayo itakaguliwa, kuzinduliwa, kufunguliwa, na kuwekwa mawe ya msingi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Shinyanga, Mwalimu Alexius Kagunze, akizungumza na Misalaba Media leo, ameeleza kuwa mwenge utapokelewa katika viwanja vya Shule ya Msingi Ibadakuli majira ya saa 12:00 asubuhi na utaanza kukimbizwa kwa umbali wa kilometa 74.5 katika Halmashauri hiyo.
Miradi Itakayozinduliwa na Mwenge wa Uhuru:
1. Ufunguzi wa Madaraja Mawili:
Mwenge utafungua rasmi madaraja mawili yaliyojengwa na TARURA, ambayo yaligharimu zaidi ya shilingi milioni 249. Madaraja haya yalikamilika mwaka jana baada ya kuwekwa mawe ya uzinduzi.
2. Shule ya Watoto wenye mahitaji maalum:
Mwenge utazindua shughuli za shule ya watoto wenye mahitaji maalumu Buhangija, ambapo serikali ilituma shilingi milioni 190 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili, pamoja na wahisani ambapo thamani ya shilingi milioni 213 imetumika katika shule hiyo.
3. Mradi wa Hifadhi ya Mazingira:
Katika kata ya Ibinzamata, mwenge utazindua mradi wa hifadhi ya mazingira ambao umegharimu shilingi milioni 2.1 na kujumuisha shughuli za ufugaji nyuki.
4. Mradi wa Maji Kijiji cha Ugayambelele:
Mwenge utatembelea na kukagua mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 279 ili kujiridhisha kama bado unaendelea kufanya kazi vizuri.
5. Ujenzi wa Soko Kuu la Shinyanga:
Mwenge utaweka jiwe la msingi katika soko kuu jipya lenye zaidi ya vibanda mia moja, mradi ambao umegharimu shilingi bilioni 1.8.
6. Shule ya Sekondari Butengwa:
Mwenge utafungua rasmi shule mpya ya sekondari Butengwa iliyopo kata ya Ndembezi iliyojengwa kwa ubora wa hali ya juu, ambapo Mkurugenzi Mwl. Kagunze ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
7. Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga:
Mwenge utaweka mawe ya msingi katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga ambapo maboresho yenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 yamefanyika kwa kukarabati majengo mbalimbali.
8. Uwezeshaji Vijana:
Mwenge utatembelea mradi wa uwezeshaji vijana ambao Halmashauri imewapatia mkopo na kuwasaidia kuandaa mazingira mazuri ya kazi.
Mkurugenzi huyo Mwalimu Kagunze amepongeza wananchi wa Manispaa ya Shinyanga kwa ushiriki wao mkubwa mwaka jana, uliowezesha Halmashauri kushika nafasi ya kwanza katika mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 kwenye Mkoa wa Shinyanga lakini pia ilishika nafasi ya sita katika kanda ya ziwa vile vile kitaifa, Manispaa ya Shinyanga ilishika nafasi ya tisa kati ya Manispaa zote zaidi ya 180 nchini Tanzania.
“Niwakaribishe sana wananchi wa Manispaa ya Shinyanga kujitokeza kushughulia mbio za Mwenge, baada ya kutembelea miradi hiyo yote, tutakuwa na mkesha usiku katika uwanja wa Sabasaba Kambarage mjini Shinyanga,” amesema Kagunze.
TAZAMA VIDEO