MFUKO wa Bima ya AfyaAHA Nchini (NHIF) mkoani Mwanza umeanza kutoa elimu ya kuhamasisha watu wasio katika makundi rasmi ya kazi kujiunga kwenye huduma hiyo kuwawezesha wananchi kuwa na uhakika wa kupata matibabu pindi wanapokumbana na matatizo ya kiafya.
Wito huo umetolewa Jijini Mwanza na Afisa Uanachama wa NHIF mkoani Mwanza, Emmanuel Nyamagomwa wakati wa zoezi la kuhamasisha watu kujiunga na vifurushi mbalimbali vinavyotolewa na Bima hiyo kwa watu walio nje ya mfumo rasmi wa ajira ili waweze kuwa na kinga dhidi ya maradhi yanayoweza kuwapata.
"Tunatembelea maeneo yote mkoani kwetu kutoa hii elimu ya Bima kwani ni mhimu kwa wananchi kupata hiyo huduma kabla ya kuugua na mtu anaweza kuhudumiwa kuanzia ngazi ya chini hadi kumwezesha mgonjwa kulazwa kwenye hospitali zs rufaa alisema Nyamagomwa.
Alisema wameamua kuhamasisha watu walio katika makundi yasiyo rasmi kujiunga na vifurushi vya Najali Afya ambavyo michango yake inaanzia shilingi 192,000 kwa mtu mmoja na wanandoa 384,000 zote kwa mwaka ili kuwawezesha watanzania wote kuwa na Bima ya Afya.
Nyamagomwa alisema wanaendelea na uhamasishaji huo kuendana na dhamira ya serikali ya kuhakikisha kuwa kunakuwa na Bima ya watu wote hapa Nchini ili jamii iweze kuzoea mfumo huo.
Mwananchi toka Kitangiri Jijini Mwanza Elias Masumba alisema anashangaa kusikia kuwa NHIF inatoa huduma hadi kwa watu walio nje ya mfumo rasmi wa kazi hivyo akaahidi kujiunga nao ili awe na uhakika wa matibabu atakapouguwa.
"Nitakata Bima hiyo kwa pamoja na familia yangu ili tuweze kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu yanapojitokeza kwani mwenye kufahamu hali ya Afya yangu kwa kesho ni Mwenyezi Mungu" alisema Masumba.
Alisema amehamasika kujiunga na Bima hiyo kwa kuwa ni kubwa kulinganisha na ile ya Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF) ambayo alikuwa akiitumia hapo awali ambayo inamwezesha mnufaika kupata huduma hadi ngazi ya hospitali ya mkoa.