Na Swedi Mbaruku, Misalaba Media
Mchezo wa nusu fainali ya pili ya Dkt. Samia
Katambi Cup 2024 umehitimishwa katika Uwanja wa Shycom, Manispaa ya Shinyanga,
huku gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki likiwa ni kurudi kwa kishindo kwa
Masekelo FC waliotoka sare ya 1-1 dhidi ya KASHUWASA na hatimaye kuibuka na
ushindi kupitia mikwaju ya penati.
Mchezo ulianza saa tisa alasiri na uliendelea
kwa ushindani mkali, huku nidhamu ya hali ya juu ikioneshwa na timu zote mbili
kutoka mwanzo hadi mwisho. KASHUWASA walionekana kuwa na udhibiti wa mchezo kwa
muda mrefu, wakionesha nia ya kufuzu kwa fainali ya michuano hii.
Hata hivyo, mchezo huo ulikuwa wa umakini
mkubwa ambapo kila kosa lilikuwa na uwezo wa kubadili matokeo. Mlinda mlango wa
KASHUWASA ataendelea kuukumbuka mchezo huu kwa kosa lililowapa Masekelo FC
nafasi ya kusawazisha kupitia shambulizi ndani ya eneo la hatari, baada ya yeye
kucheza mpira mara mbili mfululizo.
Mashabiki wa Masekelo FC walionekana
kufurahia ushindi huo, huku wakiahidi kuonesha mchezo mzuri dhidi ya wapinzani
wao katika fainali, Ngokolo FC, ambao walifuzu kwa kuwatoa Kolandoto FC kwa
goli 1-0.
"Tumefurahi
kuwatoa KASHUWASA kwani wamekuwa wapinzani wetu wa muda mrefu, walitutoa kwenye
michuano ya Ramadhani, na leo wameonja machungu tuliyopitia," alisema mmoja wa mashabiki wa Masekelo FC.
Kwa upande wake, kocha wa KASHUWASA FC
alisema kuwa licha ya juhudi zao kubwa, matokeo yalikuwa tofauti, lakini
watalenga kutoa ushindani mkubwa katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.
"Tunashukuru
tumemaliza mchezo salama. Matokeo tunayapokea kama sehemu ya mchezo, kuna
kushinda, kusare, na kupoteza. Sasa tunajiandaa kwa mchezo wa mshindi wa
tatu," amesema kocha huyo.
Mratibu wa mashindano haya, Samweli Jackson,
amesema kuwa tarehe ya mchezo wa fainali na ule wa kutafuta mshindi wa tatu
itatangazwa hivi karibuni. Pia, siku ya Jumamosi eneo la Ngokolo Mitumbani
kutakuwa na michezo ya burudani kama vile kucheza muziki na sanaa za maonyesho.
"Niwaombe
wananchi waendelee kufuatilia vyombo vya habari. Tutatangaza tarehe ya michezo
ya fainali na mshindi wa tatu hivi karibuni. Pia, siku ya Jumamosi eneo la
Ngokolo Mitumbani kutakuwa na michezo ya dance, hivyo nawasihi wenye vipaji
wajitokeze kwa wingi," amesema
Samweli.
Washindi wa Dkt. Samia Katambi Cup 2024
katika mashindano ya mpira wa miguu watapata zawadi kama ifuatavyo: mshindi wa
kwanza shilingi milioni moja, wa pili laki tano, na wa tatu laki tatu.
Kwa upande wa vikundi vya kudance, mshindi wa
kwanza atapata shilingi laki 5, wa pili laki 3, na wa tatu shilingi laki 1.
Mwisho wa kujiandikisha kwa mashindano ya dance ni tarehe 20.08.2024, siku ya
Jumanne, na kwa mawasiliano zaidi unaweza kupiga simu namba 0763715282.
Mratibu wa mashindano haya, Samweli Jackson akizungumza na waandishi wa habari.
Timu ya KASHUWASA FC.