MASEKELO FC YATWAA UBINGWA MICHUANO YA DK. SAMIA KATAMBI CUP 2024, WAKABIDHIWA SHILINGI MILLIONI SITA (6,000,000)

Na Elisha Petro, Misalaba Media

Timu ya Masekelo FC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Dokta Samia Katambi Cup baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 10-9 dhidi ya Ngokolo Stars katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Chuo cha Ualimu Shinyanga (ShyCom).

Mchezo huo ulianza kwa ushindani mkubwa ambapo Masekelo FC walitangulia kupata goli katika dakika ya 65 kupitia mchezaji wao mahiri. Hata hivyo, Ngokolo FC hawakukubali kushindwa kirahisi, kwani walifanikiwa kusawazisha goli hilo mnamo dakika ya 78, na hivyo kupelekea dakika 90 za mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1.

Katika mikwaju ya penati, Masekelo FC waliibuka washindi kwa mikwaju 10-9, na hivyo kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Kapteni wa timu ya Ngokolo FC, Charles Komanya, amewashukuru mashabiki wao kwa sapoti kubwa na pia alimpongeza Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira & Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, kwa kuandaa michuano hiyo. Aliomba michuano kama hii iendelee kuandaliwa ili kusaidia kuinua vipaji vya vijana.

"Nawaomba radhi mashabiki wetu kwa matokeo haya. Tulikuwa na lengo la kutwaa ubingwa, lakini hatukufanikiwa. Ninashukuru sana kwa michuano hii iliyokuwa ya amani, na ninamuomba Mhe. Katambi aendelee kutuunga mkono," amesema Komanya.

Kwa upande wao, wachezaji wa Masekelo FC walitoa shukrani kwa mashabiki wao kwa umoja na mshikamano waliouonyesha tangu hatua ya mwanzo hadi kuchukua ubingwa.

 Pia waliwaomba wadau wa michezo, akiwemo Mhe. Katambi, kuwekeza katika sekta ya michezo mkoani Shinyanga ili kuibua vipaji zaidi na kutimiza ndoto za vijana.

Kabla ya fainali hiyo, timu ya KASHUWASA ilishika nafasi ya tatu baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Kolandoto FC.

Zawadi zilitolewa kwa washindi, ambapo Masekelo FC walizawadiwa Shilingi Milioni 6, Ngokolo FC Shilingi Milioni 3, na KASHUWASA Shilingi Milioni 1 pamoja na seti moja ya jezi kwa kila timu iliyofika hatua ya robo fainali. 

Zawadi nyingine ni pamoja na tuzo ya golikipa bora iliyoenda kwa Laurent Luzi wa Ndembezi FC, na zawadi za wachezaji waliofunga hat-trick katika kila mchezo.

Michuano ya Dokta Samia Katambi Cup ilihusisha timu 32 kutoka maeneo mbalimbali ya Shinyanga, ikiwa na lengo la kuibua na kukuza vipaji vya vijana kupitia michezo.


Previous Post Next Post