SERIKALI KUJENGA MABWENI MAWILI ENDUIMENT SEKONDARI LONGIDO

 


SERIKALI imeamua kubeba jukumu la kujenga mabweni mawili ya shule ya sekondari ya wasichana ya Enduiment iliyopo Kijiji cha Lerangwa Kata ya Olmology Tarafa ya Enduiment wilayani Wilayani Longido Mkoani Arusha baada ya bweni moja la shule hiyo kuungua moto usiku wa agosti 26 mwaka huu.

Akizungumza na wazazi na wanafunzi wa shule hiyo,Naibu Waziri wa Madini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Longido,Dkt Steven Kiruswa alisema kuwa Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Elimu kwa pamoja wameahidi kushirikiana na kuhakikisha mabweni mawili ya wasichana na wavulana katika shule hiyo yanajengwa haraka ndani ya muda mfupi wa kipindi hiki cha likizo.

Kiruswa alisema serikali imeguswa sana na janga hilo la bweni moja kuteteketea kwa moto lililokuwa likichukua wanafunzi 340,vitanda 170 na magodoro 340 mali zote zimeteketea kwa moto na hakuna maafa na ndio maana serikali imemwagiza yeye kama Waziri kwenda katika shule hiyo kutoa pole kwa wanafunzi na wazazi na kusema kitu ambacho serikali imekiahidi kuchukua kwa haraka.

Alisema wakati serikali ikiamua kubeba jukumu la ujenzi wa mabweni mawili yeye kama Mbunge wa Jimbo la Longido kwa kushirikiana na marafiki zake tayari amechukua hatua ya kununuwa magodoro,mablangeti na shuka zenye thamani ya mamilioni ya fedha na mali hizo zote ziko katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Longido tayari kusafirishwa kwenda katika shule hiyo.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha Kupitia Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi{UVCCM],Zaytuni Swai alisema kuwa yeye aliamua kuungana na Mbunge Kiruswa kwa ajili ya kuwapa pole na kwa kuwa yeye ni mbunge wa Mkoa wa Arusha ameguswa sana na janga hilo na pia ameamua kutoa msaada kwa wanafunzi wasichana taulo za kike 500 na Blangeti 50 zote zikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja.

Swai alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inajali sana elimu na ndio maana baada ya janga hili imekuwa mstari wa mbele kuja kutoa msaada wa ujenzi wa mabweni mawili ili wanafunzi waweze kulala kama zamani.

Naye Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Longido,Gilbert Sombe alisema katika taarifa yake kuwa shule hiyo inahitajika kujengwa mabweni matatu kwa gharama shilingi milioni 390,vitanda 170 vinapaswa kununuwa kwa gharama ya shilingi milioni 142 na magodoro 340 yanapaswa kununuliwa kwa gharama ya shilingi milioni milioni 60.

Sombe alisema kuwa bweni liliungua wakati wanafunzi wanapata mlo wa jioni na baadae waende darasani kwa masomo ya jioni na ndani ya bweni kulikuwa na mwanafunzi mmoja aliyekuwa mgonjwa na walipofanya uhakiki mwanafunzi huyo alikuwa ametoka nje wakati moto ukiwaka.

Alisema hatua zilizochukuliwa baada ya moto huo kuwaka ni kuzimwa kwa haraka kwa kushirikiana na wananchi na wanafunzi na wanafunzi kuhamishiwa kwenye vyumba vya madarasa kwa malazi na Mkuu wa Wilaya ya Longido kuunda timu kwa ajili ya uchunguzi kujua chanzo cha moto.


























Previous Post Next Post